RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania,John Pombe Magufuli, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho
ya sherehe ya Siku ya Wafanyakazi Duniani,“Mei Mosi” ambayo mwaka huu kitaifa
yatafanyika,Makao Makuu ya Nchi,Dodoma.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Nicholas Mgaya, wakati jana alipokuwa na Kamati yake ya maandalizi ya
maadhimisho hayo katika kikao chao kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Jordan
Rugimbana,alisema Rais Magufuli atahudhuria maadhimisho hayo kwa mara ya kwanza
akiwa na wadhifa wa ukuu wa nchi.
Mgaya alisema Tucta waliwasilisha
maombi rasmi ya kumuomba Rais Magufuli kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo
na tayari wamepata taarifa rasmi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa Rais
amekubali kuwa mgeni rasmi.
Katika kikao hicho ambacho kilikuwa
na lengo la kujadili na kuendelea kuweka mipango na maandalizi ya kufanikisha
sherehe za mwaka huu kwa mafanikio makubwa,Mgaya alisema ni faraja kwa Mkuu
huyo wa Nchi kukubali kushiriki katika Maadhimisho hayo ambayo pia yanafanyika
Makao Makuu ya Nchi.
Alisema ili kufanikisha sherehe za
Mei Mosi, Tucta Makao makuu watachangia nusu ya gharama zote za sherehe nzima
na nusu inayobaki itachangiwa na wadau mbalimbali wakiwemo waajiri ambapo kwa
mujibu wa Kamati ya Maandalizi Bajeti nzima ya sherehe ya mwaka huu ni Sh
milioni 29.6.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa
Rugimbana aliishukuru Tucta na Serikali kwa ujumla kwa kuupa Mkoa wa Dodoma
ambao ni Makao Makuu ya Nchi heshima ya kipekee ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho
ya sherehe ya Sikukuu ya Mei Mosi Kitaifa mwaka huu.
Naye Katibu wa Tucta Mkoa wa Dodoma,
Ramadhani Mwendwa alisema tayari wameunda kamati ya maandalizi ya sherehe na
jukumu kubwa lililoko mbele ni kutafuta fedha na michango kutoka kwa wadau,
wengi wao wakiwa ni waajiri serikalini.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI