IMEFAHAMIKA
kwamba Bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano itaizidi ya iliyokuwa ya Serikali
ya Awamu ya Nne kwa Sh7.1 trilioni.
Hayo
yamefahamika baada ya Waziri wa Fedha,Dkt.Philip
Mpango, kutangaza sura ya bajeti ya mwaka 2016/17 inayoonyesha kutakuwa na
makusanyo na matumizi ya Sh29.5 trilioni.
Akiitangaza Sura hiyo ya bajeti ya mwaka 2016/17,Dkt.Mapngo,alieleza kuwa inatofautiana na iliyopita iliyokuwa ya Sh22.45 trilioni katika maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na kiwango cha fedha kitakachotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo, ambacho ni zaidi ya mara mbili ya fedha za eneo hilo katika bajeti iliyopita.
Waziri
wa Fedha, Dk Phillip Mpango alisema wakati akiwasilisha mapendekezo ya kiwango
cha ukomo wa bajeti jijini Dar es Salaam jana kuwa kati ya fedha hizo, Sh18.46
trilioni, ambazo ni sawa na asilimia 62.5 ya bajeti yote, zitatokana na jumla
ya mapato ya ndani yanayohusisha na halmashauri.
Kiwango
hicho kimezidi Sh3.64 trilioni ya bajeti iliyopita ambayo ililenga kukusanya
Sh14.82 trilioni. Ambapo ameeleza kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya
Sh15,105 bilioni, sawa na asilimia 82 ya mapato ya ndani.
Alisema
makisio ya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi yameongezeka kwa kuwa kuna
viashiria vingi vinavyoonyesha kwamba Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa kushirikiana
na wizara na taasisi zinazokusanya maduhuli, zina uwezo wa kukusanya kiasi
hicho.
Aliendelea kusema,kipaumbele cha kwanza cha
Serikali kitakuwa ni kujizatiti katika ukusanyaji wa mapato kwa kubuni vyanzo
vipya na kuendelea kudhibiti mianya mbalimbali ya ukwepaji wa kodi.
Alisema kwamba,suala hili linahitaji ushirikiano wa
karibu na wananchi ili kujiletea maendeleo ya haraka kwa kushiriki kulipa kodi
na kuwafichua wakwepa kodi kwa kuwaona kama maadui wa maendeleo ya Taifa.
Kwa
mujibu wa Dk Mpango, Sh17.72 trilioni zitakuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida,
wakati Sh11.82 trilioni, sawa na asilimia 40 ya bajeti nzima, zimetengwa kwa
ajili ya shughuli za maendeleo.
Katika
bajeti iliyopita, matumizi ya kawaida yalitengewa Sh16.7 trilioni, sawa na
asilimia 74.3 wakati shughuli za maendeleo zilipangiwa Sh5.76 sawa na asilimia
25.9.
Akongea na Waandsihi wa Habari,Mwenyekiti wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo “CHADEMA”,Freeman Mbowe,alisema asilimia 40 kwenda kwenye mipango ya maendeleo, hili ni jambo jema.
Mbowe
ambaye pia ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, alisema kupunguza matumizi ya kawaida ya Serikali na
kuelekeza fedha zaidi kwenye mipango ya maendeleo,litakuwa jambo jema pindi kama
litatekelezeka.
VIPAUMBELE :
VIPAUMBELE :
Kwa mujibu wa Dk Mpango, shughuli zitakazopewa kipaumbele kwenye mipango hiyo ya maendeleo zimegawanywa katika maeneo manne ambayo ni viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, kufungamanisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu, mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji na pia usimamizi wa utekelezaji wa mpango.
Dk
Mpango alisema washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh3.6 trilioni,
ikiwa ni ongezeko la Sh1.7 trilioni kulinganisha na Sh1.88 trilioni zilizokuwa
zinategemewa kwenye bajeti iliyopita.
Fedha
hizo zitakuwa za misaada na mikopo nafuu kutoka nje ambayo ni pamoja na GBS,
Basket Fund na miradi ya maendeleo.
Aidha
Serikali inatarajia kukopa Sh5,374.3 bilioni kutoka soko la ndani kwa ajili ya
kulipia hati fungani na dhamana za Serikali zinazoiva pamoja, wakati kutoka
kwenye soko la nje kwa masharti ya kibiashara inatarajia kukopa Sh2.1 trilioni.
Awali
Spika Job Ndugai alisema kwa mujibu wa utaratibu mapendezo hayo yalipaswa
kuwasilishwa tangu Machi 11, lakini kutokana na ratiba za wabunge wengi kuwa
kwenye majimbo yao, aliamua kuongeza siku.
Hata hivyo Spika alitoa ushauri kwa wabunge wote
kwenda kuyasoma mapendekezo hayo,ili wapate nafasi ya kuchangia bajeti
itakapowasilishwa bungeni.
Pia aliwaasa kuhudhuria kwenye vikao vyao vya
kamati,ili kujipanga vyema.Huku akionya kwa ambao hawataonekana kwenye
vikao,Ofisi ya Bunge itawasilisha majina yao kwenye vyama vyao ili wachukuliwe
hatua zinazostahili.
MIRADI YA MAENDELEO
Katika kuongeza wigo wa makusanyo ya kodi, Dk Mpango alisema sera za mapato kwa mwaka 2016/2017 itajielekeza kufanya tathimini ya mkupuo ya majengo ili kuongeza mapato.
Katika
mpango wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, Dk Mpango alisema kipaumbele
kitakuwa ni mradi wa magadi soda ulioko kwenye Bonde la Engaruka ambako utafiti
umebaini kuna magadi ya mita za ujazo bilioni 4.68 ambazo huongezeka kila mwaka
kwa mita milioni 1.9 za ujazo.
“Mradi utahusisha kiwanda cha kuzalisha tani
milioni moja za magadi kwa mwaka kwa ajili ya matumizi ya viwanda, hususan
madawa, vioo na sabuni,”
alisema.
Mradi
huo utakapokamilika utaliingizia taifa Sh 400 bilioni kwa mwaka.
Eneo
jingine ni kufufua kiwanda cha General Tyre cha Arusha, ambacho kimetengewa Sh2
bilioni kwa kazi hiyo. Pia kiwanda cha viuadudu kilichopo Kibaha mkoani Pwani
ambacho mradi wake utatekelezwa kwa awamu tatu, mbili za mwisho zikihusisha
ujenzi wa kiwanda cha mbolea na cha virutubisho.
Pia
mpango huo utahusisha uendelezaji wa viwanda vidogo mkoani Morogoro, Dar es
Salaam, Mbeya na Mwanza.
Katika
kufunganisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu, Serikali itaweka nguvu
kwenye elimu na mafunzo ya ufundi, ikihusisha kuimarisha mifumo, majengo na
miundombinu katika shule za awali, msingi na sekondari.
Pia
itahusisha ukarabati, upanuzi na ujenzi wa vyuo vikuu, mradi wa upanuzi wa Chuo
Kikuu Kishiriki cha Elimu (Mkwawa, Duce, Udom na OUT, Ardhi, Mzumbe, Sokoine,
Muhimbili, Ushirika, Chuo Kikuu cha Sayansi cha Mwalimu Nyerere na pia mikopo
ya wanafunzi wa elimu ya juu.
Eneo
hilo litahusisha uendelezaji ustawi wa jamii kwa kuangalia huduma za afya,
maji, kazi na ajira, na uwezeshaji wananchi kwa kutoa Sh50 milioni kwa kila
kijiji.
MAZINGIRA WEZESHI
Katika kujenga mazingira wezeshi, Serikali itaongeza uwezo wa uzalishaji umeme, usambazaji umeme mijini na vijijini, ujenzi wa kiwanda cha kupokea, kuchakata na kubadilisha gesi asilia kuwa katika kimiminika kwa ajili ya kusafirisha nje, ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha gesi asilia, ujenzi wa miundombinu ya usafiri, teknolojia ya habari na mawasiliano, miradi ya makaa ya mawe na mradi wa chuma wa Liganga.