BARAZA la
madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, limeikataa taarifa ya utekelezaji wa
miundombinu ya barabara kutokana na kutopita katika kamati husika, na kuzua
marumbano baina yao na mbunge wa Jimbo la Kahama,Jumanne Kishimba,aliyetaka
ijadiliwe ili kuibua ufisadi katika Halmashauri hiyo.
Katika
kikao maalumu cha Baraza hilo,madiwani walipinga kuwasilishwa kwa taarifa
hiyo,ambapo Mwenyekiti wa Kamati ya Mpango Mji na Mazingira, Bernad Mahongo, alisema
wanaitilia shaka taarifa hiyo kutokana na kutopitia katika kamati yake
kujadiliwa kabla ya kufikishwa mbele ya Baraza la madiwani.
Mahongo ambaye pia ni diwani wa kata ya
Majengo alisema taarifa hiyo haijawahi kujadiliwa na kamati yake na kwamba
irudishwe ili iweze kujadiliwa upya,kwa mujibu wa kanuni za Halmashauri
zinavyoelekeza.
Hata
hivyo Mbunge wa Jimbo la Kahama,Jumanne Kishimba,alidai kutopita katika Kamati
husika kwa hoja hiyo ni muendelezo wa ubadhirifu na ufisadi uliokithiri kwa
wataalamu na watendaji wa Halmashauri hiyo hivyo kupendekeza waijadili ili
kuibua madudu,ambayo walilenga kuyafanya,jambo ambalo lilipingwa na madiwani
kwa kusisitiza irudi katika Kamati Husika.
Kufuatia
hoja hiyo iliyoibua hofu ya wizi na matumizi mabaya ya fedha katika taarifa ya
miundombinu ya bara bara, mhandisi wa mji, Eng Job Mutagwaba, alisema suala la
miundombinu haswa ya bara bara inahitaji utaalamu mkubwa,na kama madiwani
wanahofu na utendaji kazi wao wapo tayari kuchunguzwa na Takukuru.
Hata
hivyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Anderson Msumba, alifafanua
taarifa hiyo iliwasilishwa kimakosa sambamba na kutokuwa sahihi kutokana na
kuwa ni taarifa ya
utekelezaji wa miundombinu ya mwaka 2014/15 na kwamba ilishafanyika na
ikalipwa.
“Taarifa
hii Mkuu wa Idara amejichanganya,iliishafanyika na tayari imelipwa,nawaomba
radhi, nakuahidini hali hii haitojirudia
tena,”alisema Msumba.
Madiwani wa halmashauri ya mji wa kahama walikutana
kujadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbali mbali za miradi ya maendeleo
kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2015/016.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI