EDWARD Lowassa,Waziri Mkuu Mstaafu na
aliyekuwa Kada wa muda mrefu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM),aliyejiunga CHADEMA na
kupeperusha bendera ya chama hicho kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania,kwa kivuli cha UKAWA,bado anaitesa CCM.
Lowassa ambaye alikihama CCM,akiambatana na
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga,Khamis Mgeja na makada kadhaa wa Chama
hicho tawala,amekiacha kikiwewesuka kutokana na kuanza kutimuana kwa viongozi
wa kada kadhaa za uongozi sambamba na wanachama kwa madai ya usaliti.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya ya
Arumeru,Mathias Manga,amevuliwa Ukamanda wa Vijana wa Chama hicho huku Uongozi
wa CCM wilaya ya Kahama kikiwasimamisha uanachama makada wake 135 na
kupendekeza wengine wafutwe uanachama,kwa madai ya usaliti.
Maamuzi hayo ambayo duru za siasa
zinabainisha yanatokana na wengi waliokumbwa na kadhia hiyo kuwa ni wale
walionesha kumuunga mkono,Lowassa,yanadhihirisha ni namna gani kivuli cha
mwasiasa huyo mwenye ushawishi na mvuto kuendelea kukitesa chama hicho.
Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM),mkoani
Arusha,umeomba uongozi wa CCM kumvua uongozi na kumnyang’anya kadi ya Uanachama
Manga,ambaye pia ni Mfanyabiashara maarufu wa Madini ya Tanzanite na aliwahi
kuwa Diwani wa Kata ya Mlangarini kwa tiketi ya CCM kuanzia mwaka 2010 hadi
mwaka 2015.
Pia baraza hilo linawataka makamanda wa
vijana wa wilaya za Longido,Arusha mjini na Monduli(hawakutaja majina)wajipime
wenyewe kama wanastahili kuendelea
kukalia nyadhifa hizo au wajiondoe wenyewe kabla hawajawatoa kwa aibu.
Uamuzi huo wa Baraza Kuu la UVCCM
Mkoa,ulifikiwa kwenye Kikao chake kilichokutana kwa siku tatu,kuanzia Aprili 10
mpaka 12,mwaka huu,ulitolewa na Katibu Hamasa wa umoja huo,mkoani Arusha;Nsomi.
Alisema Manga alisaliti CCM wakati wa Uchaguzi
Mkuu kwa kufanya vikao na aliyekuwa mgombea urais wa CHADEMA akiungwa mkono na
UKAWA,Edward Lowassa,huku akigawa fedha kwa vijana kwa lengo la kuivuruga CCM.
Anasema; “ Huyu(Manga)aliamua kumpa Kaisari
yaliyo ya Kaisari na sisi tunampa Mungu yaliyo ya Mungu,hivyo hakuna haja
kuendelea kuwa Mwanachama wa CCM wakati ni mnafiki na amekihujumu chama kupitia
fedha zake na ushahidi tunao mpaka wa picha.”
Aidha Kikao hicho cha Baraza la
Mkoa,kimetengua Kamati ya utekelezaji iliyoundwa mwaka 2012 pamoja na wajumbe
wake watano wanaowatuhumu kwa usaliti na kuunda Kamati mpya iliyopo chini ya
Mwenyekiti wa sasa,Lengai ole Sabaya.
Nsomi alisema baraza hilo limeitaka CCM
iwafukuze wasaliti wengine walio ndani ya chama hicho,kwani wanajulikana
kuanzia ngazi ya shina hadi taifa kabla ya uchaguzi wa ndani wa chama hicho
unaotarajiwa kufanyika mwakani ili kuepusha watu hao kuendelea kukihujumu
chama.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa
Arusha,Lengai ole Sabaya,alisema umoja huo umetoa onyo kali kwa Kamanda wa
UVCCM wa wilaya ya Ngorongoro,Bruno Kawasangi na kumtaka ajipime kama
anastahili kubaki katika nafasi hiyo kabla ya kudhalilishwa kwa kufukuzwa.
Alisema mfanyabiashara Manga hapaswi
kuvumiliwa kuendelea kukaa ndani ya CCM,kwani mbali ya kukihujumu chama hicho wakati
wa kampeni,lakini mpaka sasa anasambaza fedha katika Jimbo la Arusha Mjini kwa
lengo la kuwagawa vijana.
Hata hivyo Manga hakuweza kupatikana kujibu
tuhuma hizo licha ya jitihada kufanyika.Ambapo wilayani Kahama,Halmashauri Kuu
ya CCM mbali ya kuwasimamisha huku ikipendekeza baadhi yao wafutwe
uanachama,pia kimemzuia Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT)kuingia
katika vikao vya Kamati ya Siasa.
Mwenyekiti huyo wa UWT;Aoko Nyangusu,ambaye
pia ni Diwani wa Viti maalumu kwa kipindi cha miaka 27,amezuiwa pamoja na
wanachama Charles Nkwabi na Kisusi Ilindilo kuingia katika vikao vya Kamati ya
Siasa vya chama hicho ngazi ya wilaya.
Katibu wa CCM wilaya ya Kahama,Alexandrina Katabi,alisema
uamuzi huo umekuja baada ya kubaini kasoro za utendaji katika Kata
mbalimbali,ikiwamo hujuma iliyofanyika kipindi cha kampeni na Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015.
Amethibitisha kufukuzwa katika chama hicho
kwa mabalozi 20 wa nyumba kumi;makatibu uenezi ,uchumi na fedha 60 na wengine
20 na wenyeviti watano wa serikali za vijiji wakipewa onyo kali.
“Pamoja nao tumewafuta kazi wenyeviti kumi wa
serikali za vijiji ili kuleta nidhamu katika utendaji wa chama chetu.Diwani wa
Viti Maalum,Mary Lundalila amepewa barua ya onyo,Katibu Mwenezi wa Kata ya
Jana,Samweli Jacha amevuliwa uongozi.”
Aliendelea kusema kuwa Diwani wa
Viti maalumu Mary Lundalila,kikao Halmashauri ya Chama hicho hicho
Wilaya, iliazimia kupewa barua kali ya onyo huku Katibu Mwenezi wa kata ya
Jana, Samweli Jacha akivuliwa uongozi wake na kuongeza kuwa katibu wa CCM Kata
ya Majengo amesimamishwa kazi huku chama hicho kikitoa mapendekezo ya kufukuzwa
kabisa katika chama hicho.
Katika kikao hicho pia Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi kilipendekeza Diwani wa Viti Maalumu katika kata ya Nyandekwa Cecilia Mpemba kuvuliwa uongozi wake kwa makosa kama yale ya awali ya kukisaliti chama hicho katika uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge pamoja na Madiwani ulifanyika octoba 25 mwaka jana.
Hata hivyo Katabi alisema kuwa idadi hiyo ya Wanachama walikisaliti chama hicho inawaeza kuongezeka katika kata 56 zilizopo katika Wilaya ya Kahama kutokana na zoezi la kuwawajibisha wanachama kama ho tayari limekwishafanyika katika kata mbalimbali na vijiji vilivyopo Wilayani hapa.