MBUNGE wa zamani wa Jimbo
la Kahama,James Lembeli,amesema anamsubiri kwa hamu Rais wa jamhuri ya Muungano
wa Tanzania,John Pombe Magufuli,ili kumuelekeza yalipo majipu katika
Halmashauri za Mji wa Kahama na ile ya wilaya ya Ushetu,ambapo amekiri kuwepo
kwa ubadhirifu mkubwa wa mali za umma.
Akiongea katika mkutano
mkubwa wa hadhara uliojumuisha wabunge;Salome Makamba wa Viti Maalum(Chadema)na
Wilfred Rwakatare(Chadema) Jimbo la Bukoba Mjini pamoja na Mwenyekiti wa
BAVICHA;Patrobas Katambi,Lembeli alisema pamoja na kwamba yupo upinzani lakini
yupo tayari kumuelekeza Rais Magufuli majipu yanayoitafuna Kahama.
“Sina tatizo na CCM,bali
tatizo langu ni watu wanaochaguliwa ndani ya CCM,watu hawa ni hatari kwasababu wanatumia
fedha nyingi kuingia madarakani,lakini wanachoenda kufanya si kutetea maslahi
ya wananchi,kwakuwa Halmashauri za Ushetu na Mji nazifahamu,namsubiri kwa hamu
Magufuli nije nimuonyeshe Majipu na Vijipu uchungu atumbue,”alisema Lembeli
huku akishangiliwa na umati wa watu.
![]() |
MAKAMANDA wa CHADEMA katika Mkutano. |
Lembeli ambaye uchaguzi
uliopita aligombea Jimbo jipya la Kahama mjini na kushindwa,alisema hatua ambazo
anazifanya Rais Magufuli,alidai walizifanya kwa kipindi cha miaka kumi ya
Ubunge wake japokuwa serikali iliyokuwa madarakani ilionesha kupuuza harakati
hizo.
Hata hivyo Lembeli
alionesha mashaka ya kufanikiwa jitihada za Rais Magufuli kutokana na watu
wanaomzunguka kutokuwa waadilifu na hivyo kumuomba apate maelekezo ya kuendelea
kuwabaini wabadhirifu na mafisadi kutoka kwa watu ambao wapo nje ya CCM.
Katika hali isiyo ya
kawaida baada ya kupanda jukwaani kwa viongozi hao wa Chadema ilishuka mvua
kubwa ya ghafla,lakini wananchi hawakuweza kutawanyika bali walikuwa wakiimba
Lembeli…Lembeli…Lembeli…Lembeli,hali iliyopelekea kukolea kwa shangwe hizo ni
baada ya Mwenyekiti wa Bavicha Taifa,Katambi kushuka jukwaani na kuungana na
umati huo kuimba na kucheza.
Kwa upande wake Mbunge wa
Viti Maalumu,Salome Makamba,alishangazwa na kauli iliyotolewa na Mbunge wa
Jimbo la Kahama,Jumanne Kishimba,kuwaita Madiwani na Watendaji wa Halmashauri
kuwa ni Vimbulu,hawajitambui,wasiojua chochote kwa kushindwa kusimamia
Halmashauri.
Makamba alisema kauli hiyo
hakupaswa kuisema kwani inachochea chuki na kusababisha mgawanyiko huku
ukikosesha ari ya watendaji wa halmashauri hatua aliyodai inaweza kusababisha
kukosekana kwa maendeleo katika Halmashauri ya Mji,huku akiwataka Watendaji wa
halmashauri hiyo kutimiza wajibu wao kwa waledi na kwa kuzingatia utaalamu waliosomea.
Naye Mbunge wa Bukoba
Mjini,Rwakatare,alionesha wasiwasi wake katika wizara ya ujenzi iliyokuwa
ikiongozwa na waziri wa kipindi hicho ambaye ni Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania,kwa kuchelewa kutumbua majipu katika wizara hiyo ambapo alisema
alisema zilitolewa Bilioni 889 katika Bajeti ya 2015/2016,lakini ameshangazwa
na kitendo kilichofanyika Machi 2016 kwa kupeleka Bilioni 610 badala ya Bilioni
161 bila Bunge kupewa taarifa.
“Nina wasiwasi wa
uhamishwaji wa fedha hizo bila ushiriki wa Bunge,inawezekana zimepekwa kufuidia
madeni ya uchaguzi,kwani haileti picha nzuri kuhamisha kiasi kikubwa cha fedha
pasipo kuwashirikisha wabunge,nimuombe CAG akague na kufanya uchunguzi juu ya uhamishwaji
wa fedha hizo ili kubaini uhalali wa kuhamishwa kwa fedha hizo.”alisema
Rwakatare.
CHANZO cha Habari;- Ali Lityawi na Antony
Sollo.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI