![]() |
WAZIRI wa Afya,Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Ummy Mwalim
|
BARAZA
la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Kahama,limeiagiza Mfuko wa maendeleo ya
jamii TASAF III wilayani Kahama,kusitisha misaada inayotoa badala yake irudie
upya kuzitambua Kaya maskini,kutokana na huduma wanayotoa hivi sasa kuwanufaisha
wasio walengwa.
Agizo
hilo lilitolewa juzi katika Kikao cha Baraza
hilo baada ya Diwani wa Kata ya Malunga,Shaban Selle,kubainisha zoezi zima la
kutambua Kaya maskini katika Kata yake halikufanyika kwa ufanisi na Viongozi wa
TASAF III kwa kutoweza kuwafikia walengwa hali badala yake kunufaisha jamii
yenye uwezo.
Diwani
huyo,Sele,alisema Mfuko huo umekuwa ukiendelea kutoa fedha kwa Kaya ambazo
hazistahili na kusababisha kuwepo manung’uniko katika jamii hivyo kuona ni
vyema ukafanyika upembuzi yakinifu kubaini Kaya maskini zinazostahili kunufaika
na Mfuko huo.
Madiwani
wengine wa Kata za Kahama Mjini,Majengo na Nyasubi walidai manung’uniko hayo
pia yanapatikana katika Kata zao huku wakikosa ushirikiano wa kutosha kutoka
kwa viongozi pindi wanapowaomba kupatiwa orodha ya majina ya walengwa katika
Mfuko huo.
Aidha
Madiwani hao walishangazwa kuona usiri unaofanyika katika kuhudumia Kaya hizo
maskini kwa viongozi wanaosimamia Mfuko huo kwa wilaya nzima kutowashirikisha
Waandishi wa Habari katika majukumu yao wakati wanafahamu wanastahili kufanya
hivyo hasa kwakuwa kuna baadhi ya waandishi walipatiwa semina na Mfuko huo.
Nae
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kahama,Abel Shija, alisema ili kuondoa
manung’uniko hayo na kuhakikisha Kaya maskini zinazostahili kunufaika na Mfuko
huo ambazo kwa kipindi hiki hazijanufaika ni bora huduma hiyo ikasitishwa kwa
muda na kufanyika upembuzi yakinifu kwa wakati ndipo huduma iendelee kutolewa.
Alisema kuwa watu wamekuwa
wakigawana fedha ambao hawana sifa na pia kuna wengine wakitoka kata nyingine
kwenda nyingine kupata msaada huku wakisingia kuwa wao ni waathirika wa ugonjwa
hatari wa Ukimwi hali ambayo mfuko huo umekuwa kwa ajili ya kunufaisha watu
wachache.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Mji wa Kahama Anderson Msumba alisema kuwa ni kweli mfuko huo
umekuwa na mapungufu na kuongeza kuwa zoezi la kutambua kaya masikini
linasimamiwa na kamati za Vijiji na kata katika maeneo yanayohitaji msaada.
Hata hivyo alisema kuwa dosari hizo waliishazibaini kutokana
na zoezi la awali la kuwatambua kutofanyika
kwa ufasaha na marekebisho kupitia viongozi wa Mfuko wa Tasaf awamu ya tatu
inaendelea kufanyika kutambua Kaya maskini zinazostahili huku wakihakikisha
ambao tangu awali walistahili kupata huduma hiyo wakiendelea kupatiwa.