TAASISI zisizo za
Kiserikali nchini zimeaswa kutumia fedha za Wafadhili wapatiwazo kwa kutekeleza
miradi iliyokusudiwa kwa uadirifu ili kuzidi
kuwashawishi wahisani hao kutoa
fedha zaidi kwa ajili ya miradi ya kijamii,ambayo imekuwa kichocheo cha
kusukuma mbele maendeleo ya nchi.
Kauli hiyo ilitolewa jana
na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bukombe,James Ihunyo,wakati
akiongea na viongozi wa Shirika la Huheso Foundation,lililofika kujitambulisha
kuweka tawi lake wilayani Bukombe kwa lengo la kufanya kazi za Kijamii.
Ihunyo alisema Taasisi na
Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanamsaada mkubwa katika maendeleo ya
nchi,kutokana na kupatiwa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya
kijamii ambayo husukuma maendeleo ya nchi,hivyo ni vyema kutowakatisha tamaa
Wahisani kwa kutekeleza miradi iliyokusudiwa kwa uadirifu.
“Wafadhili kupitia
mashirika yenu,wamekuwa msaada mkubwa kwa serikali kusukuma maendeleo ya nchi,na
ili fedha hizo ziwe na tija kwa Taifa letu,ni budi kuwa waadirifu,kumbukeni
ninyi mnafika maeneo ambayo serikali bado kufika,mna mchango mkubwa wa maendeleo
katika nchi hii mnapotekeleza miradi hiyo ya Kijamii,”Alisema Ihunyo.
Alisisitiza uadirifu
katika shughuli ili kuwatia hamasa na kuwaamini wahisani wanaowafadhili fedha kwa ajili ya kusimamia miradi ya Kijamii kwa
tija ikiwemo mapambano ya UKIMWI,Malaria,Kifua Kikuu na majanga mbalimbali na
si kufuata mkumbo wa baadhi ya Taasisi ambazo zimefuja fedha za Wahisani kiasi
cha kuwakatisha tamaa.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa HUHESO FOUNDATION,Juma Mwesigwa,alimuhakikishia Mkurugenzi huyo Shirika lake
kufanya kazi kwa uadirifu ili kuleta mabadiriko yenye tija wilayani Bukombe,kwa
kutendea haki ufadhili watakaoupata kadri ya matakwa ya Mfadhili.
Alisema Shirika lake
lililoanzishwa mwaka 2009,limetekeleza kwa uadirifu mkubwa miradi mbalimbali ya
Kijamii wilayani Kahama,ikiwemo kutoa elimu za mapambano ya UKIMWI,Chakula na
Lishe,Ujasiriamali,Haki za binadamu,Pesa kwa Wote,na kuona umhimu wa kutanua
wigo wa majukumu hayo kwa kufungua tawi wilayani Bukombe.