RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli
amevunja bodi ya Hospitali ya rufaa ya Muhimbili baada ya kufanya ziara ya
kushtukiza katika Hospitalini hapo kujionea hali ya utoaji huduma kwa wagonjwa,na
kukutana na mazingira yaliyomsikitisha.
Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya
Habari na
Katibu Kiongozi,Balozi Ombeni Sefue, alisema Rais Magufuli,alichukua maamuzi
hayo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa ya Mhumbili
jana mchana na kukutana na madhila ambayo hayakumpendeza.
Rais Magufuli
alivunja Bodi hiyo jana iliyokuwa ikiongozwa na Dkt.Hussein Kidanto,ambayo hata
hivyo ilikuwa imemaliza muda wake.Na kumteua Professa Lawrence Mseru kukaimu
nafasi ya Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Mhimbili kuanzia leo.
Dkt.Kidanto aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo,amerejeshwa
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambako atapangiwa majukumu mengine.
Katika taarifa hiyo,ilisema Rais amesikitishwa na
kuhuzunishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa ambao baadhi yao aliwakuta wakiwa
wamelala chini,sambamba na uongozi kutojali na kushughulikia vifaa tiba muhimu kama
vya kufanyia uchunguzi wa magonjwa kama MRI na CT – SCAN zikiwa hazifanyi kazi
kwa muda wa miezi miwili ilhali vifaa hivyo vikifanya kazi katika Hospitali za
watu binafsi,na wagonjwa wanaelekezwa kwenda kupata huduma huko.
Aidha Balozi Sefue alisema katika taarifa hiyo kwamba,Rais
ametoa siku zisizozidi kumi na nne,kwa uongozi
mpya wa Mhimbili,kuhakikisha mashine zote za uchunguzi wa magonjwa ambazo ni
mbovu zinafanyiwa matengenezo ili kuudumia wagonjwa wanaofika katika hospitali
hiyo.
Tayari Wizara ya Fedha imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni
Tatu kwa ajili ya kazi hiyo na kulipa madeni ya ukarabati wa mashine za uchunguzi
wa maradhi mbalimbali nchini,huku Balozi Sefue akitoa agizo kwa hospitali zote
nchini kutakiwa kutenga fungu linalotokana na mapato yao kuhakikisha mashine na
vifaa tiba vyote vinafanya kazi muda wote kuhudumia wananchi.
Awali Rais Magufuli alifika katika Hospitali ya Agha Khan kumjulia hali Mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binadamu Bi Hellen Kijo Bisimba anayepatiwa matibabu na vipimo katika hospitali hiyo baada ya juzi kupata ajali katika makutano ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi jijini Dar es Salaam,kabla hajafanya ziara hiyo ya kushtukiza katika hospitali ya Muhimbili.