Monday, November 9, 2015

NI HISTORIA SAMATTA,ULIMWENGU. *Waiongoza TP MAZEMBE kutwaa ubingwa Afrika. *Wafurahia Ushindi kwa kuonesha mahaba yao kwa Tanzania *Samatta kinara wa mabao Afrika.

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO


Nyota wa Tanzania na timu ya Taifa ya Tanzania Mbwana Samatta amefunga goli moja kwenye ushindi wa magoli 2-0 iliyoupata timu yake ya TP Mazembe kwenye mchezo wa marudiano wa fainali ya vilabu bingwa Afrika dhidi ya USM Alger mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Stade TP Mazembe Lubumbashi, Congo DR.

Ushindi huo umeifanya TP Mazembe ichukue kombe la vilabu bingwa barani Afrika kwa mara ya tano lakini ikiwa ni
mara ya kwanza kwa wachezaji wa kimataifa wa Tanzania wanaokipiga kwenye klabu hiyo Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.

Samatta na Ulimwengu wameweka rekodi ya kuwa watanzania wa kwanza kunyanyua kombe la klabu bingwa barani Afrika huku nyota wengine waliong’ara zamani kwenye medani ya soka wakishindwa kufanya hivyo.




Mazembe ilishachukua kombe hilo mwaka 1967, 1968, 2009, 2010 na mwaka huu 2015 imefanya hivyo.

Kipindi cha kwanza cha mchezo huo hakikua na mashambulizi mengi kwa timu zote mbili hasa kwa upande wa TP Mazembe ambao walionekana kama wanalinda ushindi wao walioupata kwenye mechi ya awali nchini Algeria. Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa sare ya bila kufungana.

Kipindi cha pili Mazembe walianza kusaka ushindi na wakafanikiwa kupata goli la kuongonza lililofungwa na Mbwana Samatta kwa mkwaju wa penati dakika ya 75 baada ya Roger Assale kuangushwa na beki wa USM Alger akiwa kwenye eneo la hatari.

Goli hilo limemfanya Samatta kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo kwa kufikisha jumla ya magoli nane na kumpiku Bakry ‘Al Medina’ Babiker wa Al Merreikh ambaye wamekua wakichuana kwa muda mrefu.




Wakati dakika zikiwa zinaelekea ukingoni Mbwana Samatta alitengeneza goli jingine ambalo lilifungwa na Roger Assale ambalo lilimaliza kabisa ndoto za USM Alger kutwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza.

TP Mazembe wamekuwa mabingwa kwa jumla ya magoli 4-1 dhidi ya USM Alger, mchezo wa fainali ya kwanza uliochezwa Algiers, Algeria ulimalizika kwa Mazembe kushinda kwa magoli 2-1 huku mchezo wa marudiano ambao umepigwa jijini Lubumbashi, Congo DR ukimalizika kwa TP Mazembe kushinda kwa magoli 2-0.

Ubingwa huo unawapa Mazembe tiketi ya kushiriki fainali za vilabu bingwa duniani zitakazofanyika December mwaka huu nchini Japan.

TP Mazembe inaungana na mabingwa wa Ulaya Barcelona na mabingwa wa Copa Libertadores River Plate ambao tayari wamejihakikishia nafasi kwenye fainali hizo huku mabingwa wa Oceania klabu ya Auckland City pamoja na mabingwa wa Amerika Kusini Club America wakiwa tarari kwenye orodha hiyo.

Bingwa wa Asia kati ya Al-Ahli au Guangzhou Evergrande Taobao na J-League wataungana wataungana na vilabu vingine na kufanya jumla ya vilabu nane vitakavyocuana kwenye fainali hizo.
SAMATTA, ULIMWENGU, WASHINDWA KUELEZEA FURAHA ZAO BAADA YA KUTWAA UBINGWA WA AFRIKA

Kwa mara ya kwanza historia imeandikwa, watanzania wawili wamenyanyua kombe la klabu bingwa barani Afrika hawa si wengine ni Thomasi Ulimwengu na Mbwana Samatta lakini Samatta akiibuka mfungaji bora wa michuano hiyo mwaka 2015.
Lakini wachezaji hao wameshindwa kuzungumza maneno mengi kutokana na furaha waliyonayo ya kutwaa taji hilo kubwa na lenye heshima barani Afrika kwa ngazi ya vilabu pamoja na kuandika historia mpya nchini Tanzania.
“Sina hata cha kukwambia maneno yote yameniishia zaidi ni furaha tu”, amesema Samatta wakati alipozungumza na Shaffih Dauda mara baada ya mchezo wa fainali kumalizika.
“Ninafuraha sana nimetimiza ndoto zangu sina kitu kingine cha kueleza nimefurahi sana. Inawezekana kufika huku tulikofika kama mtu akiamua kujitolea kwa nguvu zote”, amesema Ulimwengu.
Kitu cha kufurahisha ni baadhi ya mashabiki wa Tanzania walikuwepo kwenye uwanja wa Stade TP Mazembe walioamua kuonesha uzalendo kwa kushona bendera ya Tanzania kwa kutumia baadhi ya vitambaa vyenye rangi tofauti na zile zinazopatikana kwenye bendera hiyo.
Baada ya Mbwana Samatta kufunga goli la kwanza alikimbia na kwenda kuchukua bendera aliyokuwa ameishika mmoja wa mashabiki hao na kuibusu. Lakini bendera hiyo ilikuwa na rangi ya dhambarau kwenye moja ya rangi zake.
Mchezo ulipomalizika Shaffih Dauda alifanya mazungumzo na shabiki aliyetengeneza bendera hiyo kutaka kujua imekuaje hadi akaamua kushona bendera hiyo yenye rangi tofauti na zile zinazopatikana kwenye bendera ya taifa ya Tanzania.
“Hii ni bendera ya Tanzania, lakini tuliishona usiku baada ya kukosa baadhi ya vitambaa lakini kwa uzalendo wetu tukaamua kushona tu bendera hata kama itakua na rangi tofauti lakini tuhakikishe tunaiwakilisha nchi yetu na kuwasapoti Samatta na Ulimwengu”, alisema shabiki huyo.
Chanzo cha Habari ni Shaffih Dauda Blog

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI