MBUNGE wa Jimbo la
Nyamagana mkoani Mwanza,Ezekiel Wenje amemshangaa Katibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi Taifa, Abdurahmani Kinana kila mara kulalamika juu ya Utendaji mbovu
wa Serikali inayotawaliwa
na Chama chake.
Wenje ambaye pia ni Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasi na Maendeleo “CHADEMA”Taifa,alitoa kauli
hiyo kwenye mkutano wa uzinduzi wa Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
katika Jimbo la Musoma Mjini zilizofanyika katika viwanja vya Shule ya
Sekondari Mara.
Mbunge huyo wa Nyamagana
alisema Kinana na chama chake hawawajibiki juu ya Serikali zaidi ya kubakia
kulalamika kuwa ndani ya Serikali kuna watendaji wabadhirifu wakiwemo Mawaziri
mizigo wanaoipeleka nchi mrama huku akiwa na nguvu ya kumshauri Rais,kwakuwa ni
Mtendaji Mkuu wa Chama kinachotawala nchi.
“Kinana yupo karibu na
Mwenyekiti wake wa CCM Taifa ambaye ni Rais wa Jamhuri wa Muungano wa
Tanzania,Kikwete ni vipi kashindwa kumshauri kuwang’oa na kuisafisha Serikali
na kashfa mbalimbali sambamba na kuboresha utendaji utakuwa tija kwa
wananchi,lakini amebakia kulalama hii ni dalili tosha wenzetu hawa wamechoka na
hawana jipya.”Alisema Wenje.
Aidha aliwaomba Wakulima
ambao hapa nchini hawana hadhi katika kilimo chao kutokana na sera mbovu za CCM
kujitambua na kuongoza mabadiriko ya kuindoa madarakani CCM kuanzia ngazi ya
Serikali ya Mitaa hadi Uchaguzi Mkuu ujao na kukichagua CHADEMA ambacho
kimepanga kuwakomboa kiuchumi Wakulima,ili watoe mchango wa maendeleo ya nchi.
“CCM inatia aibu Serikali
yake inaomba misaada hadi katika nchi ambazo Mawaziri wake wanazidiwa wingi na ufahari
wa magari na Mawaziri wetu,wameshindwaje kuboresha uchumi wetu na kumpatia kila
Mtanzania maisha bora kama si ufisadi tu wanaoufanya,”Alisema Wenje.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo
la Musoma Mjini,Vicent Nyerere alisema uongozi wa CCM umetawaliwa na ufisadi,na
upinzani una dhamira ya dhati ya kutetea maslahi ya Taifa kama ambavyo UKAWA walivyomudu
kufichua juu ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
“Tutaendelea kuwaumbua
ufisadi wao,na Januari mwaka 2015 tunakuja na sakata la sukari ambalo ni zaidi
ya Escrow,”Alisema Mbunge Nyerere.
Mbunge Nyerere alisema
hayuko tayari kuona wananchi wa Jimbo lake wakikamuliwa kwa kutozwa michango
mbalimbali ikiwemo ya maabara ilhali waliishatozwa
kodi katika bidhaa mbalimbali zikiwemo leseni za udereva,biashara,soda,sukari
na nyinginezo.
Awali akifungua mkutano
huo,Diwani wa Kata ya Nyamatare,Alex Kisirula ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya
Musoma kwa tiketi ya CHADEMA alisema jitihada zimefanyika kupitia kwa wahisani
kujenga uzio na kufanya ukarabati katika Shule ya Msingi Mwiseng,ambayo ina
wanafunzi wenye ulemavu mbalimbali .
Kisirula alisema wahisani
wameishatoa kiasi cha Shilingi kwa ajili
ya kuweka umeme zaidi ya shule tisa za sekondari jimboni humo pamoja na uzio wa
Shule hiyo ya Msingi Mwiseng ambapo zimetengwa zaidi ya Shilingi Milioni 240,huku
wakitarajia kukamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara kwa gharama ya Shilingi
Milioni 409.
CHADEMA Jimbo la Musoma
Mjini kimesimamisha jumla ya wagombea nafasi ya Uenyeviti wa Mitaa 71 wanaotarajiwa
kupigiwa kupigiwa kura Desemaba 14 mwaka huu,huku mgombea wake mmoja miongoni
mwao akiwekewa pingamizi Mahakamani na CCM kwa tuhuma za kukikashfu chama hicho
mara alipokihama mapema mwezi Oktoba mwaka huu.