Monday, November 17, 2014

MGOGORO WA WAFUGAJI NA MWEKEZAJI MAGARI TISA YACHOMWA MOTO NYUMBA 16 ZATIWA MOTO SIHA KILIMANJARO

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro,Leonidas Gama.


MAGARI tisa na nyumba 16 zimeteketezwa moto katika mgogoro ulioibuka kijiji cha Miti Mirefu , wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro
baina ya Wafugaji na Mwekezaji wa shamba la Ndarakwai chanzo kikiwa ni kugombea malisho.

Ilibainika kuwa chanzo cha uharibifu huo ni kugombea malisho  baina ya jamii ya kifugaji ya Kimasai na Mwekezaji katika shamba hilo kiasi cha  kusababisha ugomvi hata kuzua hali ya wasiwasi katika eneo hilo.

Vurugu hizo zilizuka hivi karibuni kati ya wafugaji jamii ya wamasai na Mwekezaji katika shamba la Ndarakwai, kijiji cha Miti Mirefu, wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali huku mlinzi mmoja wa mwekezaji huyo akijeruhiwa vibaya kwa risasi.

 MIONGONI mwa gari la Mwekezaji lililoteketea kwa moto


Kwa mujibu wa Mashuhuda wa tukio hilo walisema vurugu hizo zilizuka baada ya mifugo zaidi ya 300 ya wananchi wanaokaa jirani na shamba la Ndarakwai Ranchi, linalomilikiwa na Mwekezaji aliyefahamika kwa jina la Peter Jones, kukamatwa na walinzi wa shamba hilo.

Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, Israel Kileo alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 7:00 mchana, baada ya wafugaji kudaiwa kuingiza mifugo katika mashamba ya mwekezaji baada ya kukosa eneo la malisho maeneo ya vijijini.

 
 
Kileo alisema vurugu hizo zilihusisha wananchi kutoka wilaya za Longido na Siha ambapo wote kwa pamoja wanatafuta eneo la malisho huku baadhi wakidaiwa kutomtaka mwekezaji huyo ambaye anafanya utalii wa picha, kambi za watalii na kufuga wanyama kama Tembo,Twiga,Pofu na Nyani.

 ASKARI wa kutuliza ghasia wakiwa eneo la tukio



Naye mwekezaji huyo Peter Jones alielezea kusikitishwa na tukio hilo na kudai hajua sababu za msingi wala hasara iliyopatikana kwani aliondoka eneo la tukio huku akilazimika kusitisha safari za wageni zaidi ya 10 waliotakiwa kwenda kwa ajili ya utalii mwezi huu.


 MWEKEZAJI wa eneo la Ndarakwai,Peter Jones
 Kwa upande wake kiongozi wa jamii ya wafugaji eneo la Kitendeni na Miti-Mirefu, Kitasho Simeli alisema mgogoro umeibuka baada ya askari kupiga risasi baadhi ya vijana wa kimasai waliokuwa wakichunga eneo la karibu na eneo la mwekezaji.

 
 
Simeli aliongeza kusema hasira ya wafugaji ziliongezeka baada ya askari kuwapiga risasi vijana hao na kuwatelekeza porini hadi hapo walipoamua kumchukua na kumpeleka hospitali ya Kibong’oto na baadaye kuhamishiwa hospitali ya KCMC kwa ajili ya matibabu zaidi.



Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na mkuu wa mkoa huo, Leonidas Gama alisema serikali imesikitishwa na kitendo kilichofanywa na wafugaji hao na ameliagiza jeshi a polisi kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika.

Gama alisema katika tukio hilo wafugaji hao walichoma nyumba 16 za mwekezaji huyo ikiwamo kambi za watalii, magari 9 na kuvamia mashamba nane ambayo wameingiza mifugo kwa ajili ya malisho.

 Alifafanua kuwa Mwekezaji huyo alikuwa akimiliki ranchi yenye wanyama aina tofauti zaidi ya 65 ambao walikuwa wakiingia na kutoka eneo hilo na kusaidia kuliingizia pato la kigeni taifa sambamba na  kutoa ajira ya watu 76 ambazo atalazimika kuzisitisha kutokana na kusimama kwa shughuli zake.
 
Aidha kamati za ulinzi na usalama za wilaya ya Siha na Longido zitakaa meza moja ili kujadili na kufikia mwafaka wa mgogoro huo Novemba 19, mwaka huu.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI