SHIRIKA lisilo la Kiserikali la HUHESO Foundation la mjini Kahama limemteua Mwandishi wa habari wa magazeti ya Mwananchi,The Citizen na Mwanaspoti mkoani Shinyanga;Shija Felician kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wake.
Uteuzi huo ulifanywa na wanachama wa Shirika hilo la The Foundation for Human Healthy Society "HUHESO FOUNDATION" mwezi uliopita, ambapo ataitumikia nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Juma Mwesigwa,Bodi hiyo itaundwa na wajumbe kumi na itakuwa na majukumu yote ya kusimamia shughuli zote za utekelezaji wa shirika hilo ikiwa ni pamoja na kubuni mbinu mbalimbali za maendeleo.
Mwesigwa alisema Shirika hilo ambalo hujihusisha na shughuli mbalimbali za kijamii juzi lilizindua rasmi Bodi hiyo chini ya Mwenyekiti wake Felician ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Shinyanga {SPC}aliahidi mambo makubwa ya kuliendeleza shirika hilo katika kipindi chake cha miaka mitatu ya uongozi.
Katika bodi hiyo pia yumo Avelina Ndakama ambaye ni Makamo Mwenyekiti wa Bodi,pamoja na Atufigwege Mwakyaki ambaye atakuwa Mweka Hazina wa Bodi katika kipindi hicho cha miaka mitatu.
Bodi hiyo inaundwa na wataalamu mbalimbali kutoka sekta za serikali na binafsi wakiwemo madaktari,maendeleo ya jamii,walimu pamoja na wanasheria ambao watakuwa na kazi ya kumshauri Mwenyekiti juu ya mikakati ya kuliendeleza shirika hilo.
Shirika hilo la HUHESO Foundation katika mwaka wa fedha 2013/14 limetekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi kwa kuwaondoa katika biashara ya ngono wasichana ambao tayari wamepatiwa elimu ya ujasiriamali.
Pia Shirika hilo mbali na kutekeleza miradi ya mapambano ya maradhi ya Ukimwi pia hujishughulisha na miradi mingine ya chakula na lishe sambamba na utetezi wa haki za watoto na wanawake.