KATIKA kuhakikisha mauaji
ya vikongwe yanayoitia doa jamii,wanakijiji cha Mwakata katika Kata ya Mwakata
wilayani Kahama wameanzisha kampeni ya kuwafichua wahusikao na vitendo hivyo
dharimu.
Wanakijiji hao waliamua
kukabiliana na vitendo hivyo ili kunusuru vikongwe vinakatwa mapanga kwa imani
za kishirikina kwa kuanzisha kampeni ya
kupiga kura kwa lengo la kuwatambua
miongoni mwao wahusikao na vitendo hivyo.
Wakizindua Kampeni hizo
mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya Kahama chini ya Mwenyekiti wake
Mkuu wa wilaya hiyo Benson Mpesya,Mtemi wa Walinzi wa Jadi “Sungusungu”,Machimu
Ndalo alisema tatizo la wanawake vikongwe kuuawa katika eneo hilo ni kubwa.
Ndalo alisema kwa kipindi
cha mwaka huu,tayari watu wanne wameuawa kwa kukatwa mapanga huku sababu kubwa
ikielezwa ni imani za kishirikina,hali ambayo ikiendelea kufumbiwa macho ni
hatari kwa Taifa.
Aidha alibainisha
mazingira ya mauaji hayo kwa asilimia kubwa huanzia kwenye familia kutokana na
migogoro ya mbalimbali ya urithi wa mali,mipaka ya ardhi na elimu haba juu ya
afya inayopelekea katika kuamini ushirikina.
Hivyo serikali ya kijiji
imeamua kukabiliana na mauaji hayo ambayo yanalitia doa kubwa eneo hilo hasa
kutokana na tukio la mauaji ya kikongwe kuuawa kwa kucharangwa mapanga siku
saba tangu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Ally Nassoro Rufunga kufika kijijini hapo
na kukemea mauaji hayo.
Kwa upande wake Mkuu wa
Wilaya ya Kahama Benson Mpesya,aliwaomba wanakijiji hao kupiga kura kwa
uangalifu mkubwa pasipo kumuonea mtu,kufanyiana fitina za kukomoana ama
kulipiana visasi vinavyotokana na mikwaruzo ya kawaida kati yao ndani ya jamii.
Mwenyekiti huyo wa Kamati
ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Kahama,aliagiza mara baada ya upigaji kura
majina hayo yafikishwe kwa wakati katika Serikali ya wilaya ambayo nayo
haitafanya ajizi kuyafanyia kazi.
“Majina ambayo yataonekana
kupata kura nyingi ndio yatakayoanza kufanyiwa uchunguzi kwa kina yakifuatiwa
namengine,na sheria itachukua mkondo wake kwa watakaobainika kuhusika na
matendo hayo,”Alisema Mpesya.
Wilaya ya Kahama vitendo
vya mauaji ya vikongwe kwa kukatwa mapanga vimeshamiri huku Kijiji cha Mwakata
katika Kata ya Isaka kikiongoza kutokana na kila mwaka kupatikana kwa kikongwe
kinachoawa kwa kukatwa mapanga.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI