Tuesday, January 11, 2011

AZUIA MAITI YA MTANI WAKE ISIZIKWE

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO

Halikuwa jambo rahisi,na hakuna yeyote aliyekuwa amehudhuria maziko ya Marehemu Mzee Zacharia Kaseko aliyetarajia kukutana na kushuhudi kioja chenye kutisha katika msiba huo.

Tukio hilo la kuogofya lililofanyika wakati wa maziko huku msingi mkubwa ukiwa ni utani wa jadi,ambao ulitendwa na Mzee wa kabila la Kingoni,Andrew Chitete(74)haujapata kutokea kwa takribani robo karne iliyopita pale alipoamua kutumbukia kaburini na kukumbatia sanduku la marehemu Kaseko ambaye kabila lake ni Msumbwa na kuzuia kaburi lisifukiwqe hadi pale watani wake walipompatia fedha ndipo alipotoka kaburini na mwiliwa marehemu kuzikwa.




Hakika kitendo hicho cha kutisha alichofanya Mzee Chitete mkazi wa Kitongoji cha Kasela Kata ya Malunga kimekuwa gumzo na huenda ndicho kimekuwa cha kusisimua na kufungia mwaka 2010 kutokana na kutokea Novemba 2,2010 na kuukaribisha mwaka 2011.

Akizungumzia kioja hicho Mzee Chitete alidai si mara ya kwanza kufanya utani kama huo kwa makabila ambayo ana hakika ana utani nayo wa jadi na lengo lake ni

kudumisha mila ambayo kizazi cha sasa kinapuuzia kwa kuiga utamaduni wa kigeni.

"Ni vyema tukumbuke utani wetu wa jadi,ambapo Wazee wetu wa zamani walikuwa wakiutenda pasipo kupotosha ambapo katika misiba ilisaidia kupunguza machungu ya Wafiwa,"Alisema Mzee Chitete.

Alifafanua utani kama alioutenda katika maziko ya Mzee Kaseko aliwahi kuutenda katika maziko ya mama yake na Jaji Ihema katika Kata ya Isagehe,ambapo alitwaa Mishumaa yote na kuzuia maiti isizikwe katika kaburi liloandaliwa kwa madai ameandaa usafiri wa kuipeleka Songea kuizika,hadi alipochangiwa pesa ndipo aliporuhusu maiti izikwe na ndivyo ilivyokuwa katika maziko ya Marehemu Mzee Kaseko.

"Utani unatambulika Kisheria ndio maana katika Maziko ya mzazi wa Jaji Ihema ilipotaka kutokea vurugu kwa baadhi ya wasioelewa utani kutaka kunishushia kipigo,Jaji aliwazuia kwa kuwaeleza kuwa nina haki na kuwa ni miongoni mwa waliochanga pesa ili niruhusu maiti izikwe,"Alisema Mzee Chitete.



Alikanusha kuitumia misiba ya makabila ya Watani wake kama ni miongoni mwa mradi wa kumuingizia kipato kwa kubainisha kuwa pesa anazo changiwa pindi anapozuia maziko huzitumia kununua bidhaa mbalimbali kama Mchele,Unga, Chumvi,Sukari,Dagaa,Maharage na vinginevyo ambavyo huvipeleka kuwapa pole Wafiwa.

Mzee Chitete alisema ni ada yake kufanya utani kwa Mtani wake katika mazingira yoyote yale,wakati wa raha,wa kawaida ni vipindi vya misiba na kukisisitizia kizazi kilichopo kuuenzi Utamaduni wa makabila yetu kwa kutokuwa Watumwa wa fikra kwa kuthamini Mila na Desturi za Ughaibuni na Ulaya.

MWISHO

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI