Maamuzi na maelekezo
ya Waziri wa wa Ardhi,Nyumba na Makazi,Wiliam Lukuvi,aliyoyatoa kwa Halmshauri
ya Mji wa Kahama,imeshauriwa
yatekelezwe kwa haki.
Katika ziara aliyofanya hivi karibuni
wilayani Kahama,kwa lengo la kutatua migogoro ya ardhi iliyokuwa imekithiri
mjini Kahama na kusababisha kuwepo kwa kero ya muda mrefu kwa wananchi,Waziri
Lukuvi alitoa maelekezo kadhaa kwa viongozi wa Halmashauri ya Mji na Serikali
ya wilaya,.
Baadhi ya wananchi wakiongea kwa
nyakati tofauti na maeneo mbalimbali ya mji wa Kahama, walipongeza utaratibu wa
Waziri Lukuvi,kushughulikia migogoro ya ardhi kwa uwazi na kuomba serikali ya
wilaya kutekeleza kwa haraka maagizo yake.
Mkazi wa Kata ya Malunga,Masumbuko
Henry,alisema anampongeza Waziri Lukuvi kufika kushughulikia migogoro ya
kipindi kirefu iliyokuwa kero,huku mingi ikiwa imesababishwa na watendaji katika
Idara ya ardhi.
Aidha mkazi wa Mtaa wa Majengo,Nusura
Maganga,alisema kuhusu eneo la soko la wakulima ambalo kwa kipindi kirefu
limekuwa katika utata juu ya haki ya umiliki,ni vyema likapangiwa matumizi
haraka ilisaidie kuipa mapato Halmashauri ya Mji wa Kahama.
Maganga aliiomba halmashauri ya mji wa
Kahama inapaswa kuwaita na kuketi na wajasariamali ambao tayari waliishawekeza
kwa kujenga vibanda vya biashara katika eneo hilo lililokuwa na utata wa
umiliki uliosababisha kuikosesha mapato halmashauri.
Nae Salome Hussein mkazi wa Kata ya
Nyasubi,aliomba halmashauri ya Mji kutumia fursa hiyo kuwaweka hapo wamachinga
ambao wamekuwa wakizagaa mitaani kwa kufanya biashara katika maeneo yasiyokuwa
rasmi.
Mmoja wa Mmachinga,John
Samweli,alipendekeza eneo hilo lililokuwa la soko ni vyema likatumika kwa
bidhaa za nguo za mitumba,vyombo na biashara ndogondogo nyingine kama ilivyo
kwa wafanyabiashara waliopo Makoroboi Jijini Mwanza.
“ Nampongeza Lukuvi kuliresha eneo
hilo serikalini ambalo baadhi ya wajanja wachache walikuwa wamejimilikisha na
kujinufaisha na kusababisha kuikosesha mapato Serikali kupitia zaidi ya vibanda
100 vilivyojengwa kwa zaidi ya miaka 15 iliyopita,”alisema Samweli.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Mji wa Kahama,Anderson Msumba alisema atahakikisha anasimamia
haki baada ya eneo hilo kurejeshwa chini ya Halmashauri yake ili liweze
kusaidia kuongeza vyanzo vya mapato ya Serikali.
Msumba alisema kwa upande wa
Wajasiriamali waliowekeza kwa kujenga vibanda vya biashara alisema atakaa nao
na kuhakikisha anatenda haki ili Halmashauri na serikali zipate
mapato ambayo yatasaidia katika suala la maendeleo.