C
C |
hama cha ACT – Wazalendo,kimedhamiria kufungua kesi mahakamani kupinga uwepo wa mamlaka moja ya kutoa Takwimu za Taifa.
Kiongozi Mkuu wa chama
hicho, Zitto Kabwe amesema watafungua kesi mahakamani kupinga baadhi ya vifungu
vilivyomo katika Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari nje
ya kitengo cha upelelezi wa makosa ya kifedha kilichopo Kamata, Kariakoo jijini
Dar es Salaam, Zitto amesema haiwezekani kukawa na mamlaka moja ya kutoa
takwimu.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma
Mjini amesema tangu kutungwa kwa sheria hiyo imekuwa ikipigiwa kelele kutokana
na kuminya uhuru wa wananchi kuchambua takwimu.
"Tunataka kufungua kesi
mahakamani kupinga sheria ya takwimu kuzuia watu kuchambua, huko ndiko ukweli
utajulikana na wananchi watajua sheria hii ilivyo. Hii itakuwa kesi ya kwanza
kwa sheria hii kupelekwa mahakamani," amesema Zitto.
Amesema, "Tuna taarifa ambazo
hatukuzitoa, tukifika mahakamani tutazitoa na NBS- (Ofisi ya Taifa ya Takwimu)
haiwezi kusema una hatia au la kwa kuwa wao si Mahakama. Sisi tulitumia takwimu
zao kuchambua na tumewaeleza polisi kwamba tutawaeleza zaidi tukifika
mahakamani."
Zitto ametoa kauli hiyo siku moja
baada ya jana Jumapili Novemba 5,2017 Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk Albina Chuwa
kusema mtu mwenye mamlaka ya kutoa takwimu ni ofisi hiyo pekee.
Dk Chuwa katika kipindi maalumu
kilichorushwa na kituo cha televisheni cha Azam kuhusu miaka miwili ya utawala
wa Rais John Magufuli aliyeingia Ikulu Novemba 5,2015 alisema takwimu za Taifa
ni lazima ziheshimiwe na si kila mtu anastahili kuzitoa.
Zitto akizungumzia tuhuma za uchochezi
zinazomkabili amesema, “Nimeripoti leo kama nilivyotakiwa lakini nimeelezwa
nirudi tena Ijumaa Novemba 17,2017 wanadai wanasubiri chaji kutoka kwa DPP
(Mkurugenzi wa Mashtaka) na baada ya hapo wataona kama watanipeleka mahakamani
au la.''
"Lakini kesho, mimi nitakuja hapa
(kitengo cha uhalifu wa makosa ya kifedha) saa tatu au saa nne kama
nilivyotakiwa. Mtakumbuka natuhumiwa kwa kesi mbili ya sheria ya takwimu na
makosa ya mitandao," amesema.
Zitto pia amezungumzia uamuzi wa Jeshi
la Polisi la kuiita kamati kuu ya ACT- Wazalendo akisema haina uwezo huo na wao
kama walivyoeleza jana katika mkutano na waandishi wa habari watawakilishwa na
Mwenyekiti wa chama hicho, Yeremia Maganja na Katibu Mkuu Doroth Semu.
"Polisi hawana uwezo wa kuihoji
kamati kuu, ndiyo maana mwenyekiti na katibu mkuu wapo hapa wanaendelea na
mahojiano... huwezi kuwaita wajumbe wote wa kamati kuu kwa kuwa mtendaji wa
chama ni katibu mkuu na msemaji ni mwenyekiti na ndicho tumekifanya,"
amesema.