Mchezo huu unatarajiwa kuwa na ushindani wa hali ya juu kutokana na
timu hizo kuwa katika nafasi sawa ya msimamo wa ligi licha ya Simba
kuongoza kwa idadi ya mabao ya kufunga, huku kila moja ikihitaji kukaa
kileleni.
Mechi hii inatarajiwa kuwa ni ya vita na kisasi kutokana na hali jinsi
ilivyo katika mechi husika ambapo kila upande utahitaji kufanya vyema.
Imekaa vibaya kwa upande wa makocha wa timu zote mbili, kutokana na
historia za timu hizo ambapo mara nyingi makocha wamekuwa wakifungashiwa
virago vyao pale wanapofungwa na wapinzani wao.
Hivi karibuni kulizuka uzushi juu ya Yanga kutaka kumuondoa kocha wake,
George Lwandamina kutokana na matokeo mabaya katika mechi za awali
jambo ambalo uongozi wa klabu hiyo ulikanusha, lakini waswahili husema
lisemwalo lipo, hivyo mechi hiyo inaweza kuwa katika wakati mgumu kwa
upande wake.
Vilevile kwa upande wa Simba, Kocha Joseph Omog amekalia kuti kavu kwa
muda mrefu kutokana na uongozi wa klabu hiyo kutaka kumuondoa kutokana
na madai ya kutokifundisha vyema kikosi hicho kwa kuona kuwa kimemzidi
uwezo, lakini mkataba aliosaini umeonekana kumbeba kutokana na baadhi ya
vipengele kuwabana waajili wake.
Hivyo basi, mechi hii ndiyo itakayotoa maamuzi juu ya kuendelea kuwepo
katika kikosi hicho kwa kuwa inadaiwa kuna kipengele alichosaini
kinaeleza kuwa iwapo t i m u haitaongoza msimamo wa ligi, itawapa nguvu
viongozi kuweza kuvunja kandarasi hiyo.
Mshambuliaji wa Simba, Haruna Niyonzima akiopambana na wachezaji wa Simba.
Hivyo, atakuwa na kibarua kigumu kuhakikisha anafanikiwa kushinda mchezo huo ambao utakuwa na upinzani mkubwa.
KILA TIMU ITAHITAJI KUKAA KILELENI
Simba na Yanga zimefungana katika msimamo wa ligi kutokana na zote kuwa
na pointi 15, huku Simba ikiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mabao ya
kufunga. Simba ina mabao 19 na Yanga ina mabao 10.
Hivyo, kutokana na jinsi msimamo ulivyo, timu ambayo itashinda katika
mchezo huo ndiyo itakayopata nafasi ya kuongoza msimamo wa ligi na iwapo
itatokea wakatoa sare na Mtibwa Sugar yenye pointi 15 ikishinda mechi
yao ya Jumapili dhidi ya Singida United basi itakaa kileleni.
KUONYESHANA UBORA WA VIKOSI
Kila timu inajinadi kuwa na kikosi bora ambacho imekisajili msimu huu,
hivyo mashabiki wanasubiri kwa hamu kubwa kuona timu gani itaonyesha
ufundi zaidi katika mchezo huo.
AJIBU, NIYONZIMA & OKWI VIVUTIO
Kwa sasa habari ya mjini katika timu hizo ni kuhusiana na viwango vya
wachezaji Ibrahim Ajibu wa Yanga na Haruna Niyonzima na Emmanuel Okwi
wa Simba, hivyo kila mmoja atahitaji kuona wanafanya nini katika mechi
hiyo ya kesho.
Kwa upande wa Okwi, ndiye mchezaji kinara wa mabao kwenye ligi akiwa na
mabao nane ambayo yameifanya kikosi hicho kukaa kileleni kwa tofauti
ya mabao.
Aidha, wachezaji Ajibu na Niyonzima, kwa sasa ni gumzo kutokana na
viwango wanavyoonyesha. Mashabiki wa timu hizo wamekuwa wakirushiana
maneno huku wale wa Yanga wakidai Simba wamepoteza mchezaji (Ajibu)
kwani amekuwa muhimu Jangwani na Niyonzima akipondwa kwa kuonyesha
uwezo wa kawaida tofauti na ule aliokuwa akionyesha Yanga.
HOFU YA MASHABIKI
Hofu kubwa ya mashabiki kuelekea mchezo huo, itakuwa namna ya kuingia
uwanjani kwani kwa muonekano wa haraka Uwanja wa Uhuru jinsi ulivyo
hauwezi kukidhi mahitaji ya mashabiki kutokana na udogo wa uwanja huo
tofauti na ule wa Taifa ambao ni mkubwa.
Kuna uwezekano mkubwa kwa mashabiki wengi kuangalia mpira huo kupitia
runinga kutokana na kushindwa kuingia uwanjani licha ya kuhitaji
kuwaona wachezaji ‘live’ uwanjani.
Ni pambano la lawama kutokana na desturi la timu hizo kongwe katika soka la Tanzania,kutowaacha salama,Makocha,Viongozi ama wachezaji wa timu hizo pasipo kutupiwa hujuma za usaliti,pindi timu mojawapo inaposhindwa.
Pambano hilo si ajabu likatoa mwelekeo la mmoja wa makocha wa timu hizo,kutosherehekea sikukuu ya Krismas,akiwa katika timu itakayoshindwa katika mchezo wa kesho.
MAKOCHA KUTETEA VIBARUA VYAO
Yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo yanatarajiwa kuifanya mechi hiyo kuwa ni ya vita na kisasi.