TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU )imejinasibu kuendelea kukamilisha orodha zaidi ya watuhumiwa
wa Uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow,watakaopandishwa kizimbani.
Takukuru imejinasibu hivyo ikiwa ni siku moja baada ya wafanyabiashara Harbinder Singh Sethi na James Rugemalira kufikishwa mahakamani na kunyimwa dhamana.
wa Uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow,watakaopandishwa kizimbani.
Takukuru imejinasibu hivyo ikiwa ni siku moja baada ya wafanyabiashara Harbinder Singh Sethi na James Rugemalira kufikishwa mahakamani na kunyimwa dhamana.
Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa Takukuru Makao Makuu, Mussa Misalaba,
alisema kwa sasa uchunguzi unaendelea kwa kila aliyehusika, na hatua
zitachukuliwa kwa kadri ushahidi utakavyokusanywa.
"Mtu anaweza kutuhumiwa, lakini bila ushahidi huwezi kumshtaki,"
alisema. "Kama mtu ametuhumiwa na hakuna ushahidi ni vigumu kumkamata
ila tunaendelea kukusanya ushahidi na tukijiridhisha tutawakamata.
"Wafanyabiashara waliofikishwa mahakamani ni mwanzo tu, tunaendelea na
uchunguzi wetu na kadri tutakapokuwa tunapata ushahidi (watuhumiwa)
watahojiwa na kufikishwa kwenye mamlaka husika."
Sethi na Rugemalira walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
juzi wakikabiliwa na makosa mbalimbali, ikiwamo uhujumu uchumi ambayo
mahakama hiyo haina mamlaka ya kuyasikiliza hivyo haiwezi kutoa dhamana
na washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote.
Wafanyabiashara hao wanakabiliwa na makosa sita likiwamo la
kuisababishia serikali hasara ya dola za Marekani 22,198,544.60 (Sh.
bilioni 309.4).
MAAZIMIO NANE
Kufikishwa mahakamani kwa wafanyabiashara hao kunaonekana kama mwanzo wa
utekelezaji wa maazimio ya Bunge ya miaka mitatu iliyopita.
Mwaka 2014, wakati Bunge likijadili sakata la akaunti ya Tegeta Escrow,
lilitoa maazimio nane likiwamo la Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo
vingine vya ulinzi na usalama vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa
sheria dhidi ya watu wote waliotajwa na taarifa maalum ya kamati ya
Bunge, kuhusika na vitendo vyote vya jinai kuhusiana na miamala ya
akaunti hiyo na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi wa
sakata hilo.
Pendekezo la pili la Bunge ni serikali kuangalia uwezekano wa kuichukua
mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Shirika la Ugavi wa
Umeme (Tanesco) kwa mujibu wa sheria za nchi.
Jingine ni kufanya mapitio ya mikataba ya umeme ambalo liliitaka
serikali ilitekeleze mapema kwa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wake
kabla ya mkutano wa bajeti ya mwaka wa fedha 2015/16.
Bunge pia liliazimia serikali iandae na kuwasilisha muswada wa
marekebisho ya sheria inayounda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi
mahususi itakayoshughulikia kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa
kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi,
kijamii na kisiasa. Kipindi hicho kulikuwa na Taasisi ya Kuzuia Rushwa
(Takukuru).
Chombo hicho cha kutunga sheria pia kiliazimia Rais aunde Tume ya Kijaji
ya kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya majaji Aloysius
Mujulizi na Jaji Prof. Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Azimio la sita lilikuwa mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi
kuitaja Benki ya Stanbic na benki nyingine itakayogundulika kufuatilia
uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa
fedha zilizotolewa katika akaunti ya Tegeta Escrow kuwa ni taasisi zenye
shaka ya utakatishaji fedha haramu.
Bunge pia liliazimia Waziri wa Nishari na Madini, Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu
wa Wizara ya Nishati na Madini na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa
Tanesco wakati huo, wawajibishwe kwa kuishauri mamlaka ya uteuzi
kutengua uteuzi wao.
Azimio la mwisho ni Kamati za Kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka
kwa kuwavua nyadhifa zao kwenye kamati husika viongozi wake waliobainika
kukiuka maadili kwa kujihusisha kwa vyovyote vile na uchotaji wa fedha
za akaunti hiyo kabla ya kuanza kwa mkutano wa Bunge uliokuwa unafuata.