WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka
maofisa wa Mamlaka ya Kodi ya Mapato Tanzania (TRA),kuhakikisha wanajipanga kusanya
kodi za majengo,kwa
kuzingatia sheria,ifikapo Julai Mosi mwaka huu.
Kaonya maafisa hao kutumia weledi mkubwa
katika makusanyo hayo,na kaonya wasitoze kodi ya majengo wazee wenye umri zaidi
ya miaka 60.
Waziri Mkuu ameagiza “TRA” ijipange
kukusanya kodi za majengo kuanzia Julai mosi 2017.Huku akisisitiza utekelezaji
jukumu hilo,sheria za nchi na za ukusanyaji mapato zitamalaki.
Amesema, “Tusisikie mnawadai kodi ya
majengo wazee wenye umri zaidi ya miaka 60 kwa majengo wanayotumia kama makazi
yao.”
Waziri Mkuu;Majaliwa,alitoa agizo hilo
jana wakati akizungumza na wananchi na viongozi wa Wilaya ya Chato
waliohudhuria uzinduzi wa jengo la TRA wilayani humo mkoani Geita.
Waziri Mkuu amewataka moafisa hao
wakusanye kodi ya majengo kwenye maeneo ya mjini na siyo vijijini kwani kodi
hiyo haiwahusu.
“Msiende vijijini. Nyumba za nyasi au
za tembe hazihusiki. Tembeleeni nyumba za mijini. Piteni kwenye mitaa,
muainishe aina zote za nyumba zinazostahili kulipiwa kodi. Mkishafanya sensa,
wekeni utaratibu wa kuwawezesha wananchi kulipia kodi hizo,” alisema huku
akishangiliwa.
Pia aliwataka wananchi wanaonunua
bidhaa wadai risiti lakini wahakikishe wanapewa risiti yenye kiwango halisi
walicholipia.
“Ukipewa risiti uiangalie kama ina
kiwango halisi cha fedha uliyotoa.Kuna watu wachache wasio waaminifu wanaamua
kukupa risiti, lakini imeandikwa bei ndogo kuliko ile uliyolipia, ukitoa laki
moja anakupa risiti ya shilingi elfu kumi,” alieleza.
Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi
wa jengo hilo la ghorofa moja, Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kicheere alisema
ujenzi huo ulianza Julai 12, mwaka jana na ulikamilika Juni 12, mwaka huu.
“Ujenzi wa jengo hili umegharimu Sh
bilioni 1.4 na ulichochewa na ongezeko kubwa la idadi ya walipakodi wa Chato
kutoka watu 150 mwaka 2010/11 hadi kufikia watu 600 mwaka 2016/17,” alieleza.
Pia alisema wamejenga ofisi hizo ili
kuwapunguzia umbali wafanyabiashara wa wilaya hiyo ambao walilazimika kwenda
Geita mjini kupata huduma za TRA ambako ni umbali wa zaidi kilometa 120.
Alisema hivi karibuni watakamilisha
ukarabati wa ofisi za mikoa ya Mara, Iringa ikiwemo kujenga ofisi kwenye mikoa
mipya ya Simiyu, Katavi, Njombe na Manyara. “Pia tutajenga ofisi kwenye mkoa
mpya wa kikodi wa Kahama,” alieleza.
Alizitaja wilaya ambazo ziko mbioni
kupatiwa ofisi zake kuwa ni Kondoa, Longido, Bunda na Arumeru. Alisema katika
mwaka ujao wa fedha, TRA imelenga kukusanya Sh trilioni 17.106 na watahakikisha
wanafikia lengo hilo.