Sunday, October 23, 2016

SAMIA;'WANAWAKE ...CHUKIENI NA KUFICHUA WALA RUSHWA"

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO

JITIHADA za wanawake kujikwamua kiuchumi,licha ya kuonekana wanajituma katika shughuli za
ujasiriamali ili kuinua vipato vya familia zao zinakwamishwa na vitendo vya rushwa,imefahamika.

Makamo wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameonesha kukerwa na vitendo hivyo vya rushwa na kuwataka wanawake wajasiriamali kufichua kila aina ya rushwa wanazoombwa na wenye mamlaka katika sekta ya biashara nchini.

Alisema hayo jana wakati akifungua kongamano la wajasiriamali wanawake lililoandaliwa na Mtandao wa Sauti ya Wajasiriamali Wanawake Tanzania (VOWET) na kuhudhuriwa na wanawake zaidi ya 500.

Alisema iwapo wanawake wakiwafichua waombaji wa rushwa wanaokwamisha harakati zao za kusonga mbele kibiashara, itaiwezesha serikali kuondoa kero hiyo.

Samia alisema baadhi ya wanawake wanaombwa rushwa za ngono na nyinginezo na hukaa kimya bila ya kulifikisha suala lao hilo kwa mamlaka husika ili wasaidiwe na kwamba kukaa kimya kumechangia kuendelea kuwepo kwa kero hiyo.

Amewahakikishia wanawake hao kuwa serikali itakuwa ikiwapa kipaumbele kwenye malipo ya fedha za zabuni ili waweze kusonga mbele zaidi na kuongeza kuwa wapo wanawake ambao wamekuwa wakijikita zaidi kwenye biashara, lakini wanakumbwa na changamoto mbalimbali ikiwamo hiyo ya kucheleweshewa fedha zao.

Akizungumzia kuwaunganisha wanawake na masoko, alisema ofisi yake inashughulikia kutengeneza mtandao utakaotangaza kazi zote za wajasiriamali wanawake kirahisi zaidi.

Alisema wapo wajasiriamali wa nje ya nchi, lakini wakitaka kufahamu fursa za biashara zinazofanywa na wanawake wanashindwa kupata taarifa zao na kuwahakikishia kuwa ofisi yake inalitatua tatizo hilo.

Rais wa Vowet, Maida Waziri katika hotuba yake alimueleza Makamu wa Rais kuwa malipo ya kodi kwa makadirio ya nyuma yanakwamisha maendeleo ya wanawake nchini.

Alimuomba Makamu wa Rais kuwasaidia kufutwa kwa mfumo huo kwa kuwa licha ya kuwaathiri wajasiriamali kiujumla ila wanawake wanaathirika zaidi kwa kuwa wanalipa fedha ambazo hawana taarifa nazo.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI