MKUU wa wilaya ya
Kahama,Fadhili Nkurlu,amewaagiza viongozi wa dini kuunda Kamati ya Amani,kusudi
washirikiane na Serikali kukabili na kutokomeza mauaji ya vikongwe kutokana na
imani za kishirikina,yaliyokithiri wilayani Kahama.
Agizo hilo alilitoa juzi
katika Baraza la Iddi,lililofanyika kimkoa wa Shinyanga,wilayani Kahama katika
ukumbi wa Halmashauri ya Ushetu,ambapo aliwaomba viongozi wa dini kutoa
ushirikiano kwa serikali katika mapambano dhidi ya mauaji ya vikongwe,ambayo
yanarejea kwa kasi wilayani Kahama.
Nkurlu alisema ni vyema
Kamati hiyo ikaundwa kwani itakuwa
msaada mkubwa wa kudumisha amani,kutokana na kuunganisha viongozi wa dini
kutoka madhehebu mbalimbali na kuomba kazi ya kwanza kuifanya ni kuhakikisha
wanawaasa waumini wao juu ya athari ya kuua vikongwe kutokana na imani za
kishirikina.
“Mauaji ya vikongwe
yanarejea kwa kasi wilayani petu,wiki hii pekee vikongwe vine vimeuawa katika
Kata za Chambo,Iyenze,kijiji cha Nyashimbi Kata ya Mhongolo,na leo hii Kikongwe
ameuawa Kata ya Segese,na imani viongozi wa dini mkiingilia vita hivi
tutakomesha mauaji hayo,”alisema Nkurlu.
Aidha Nkurlu alisema
kuundwa kwa kamati hiyo kutazidisha amani kwa kuondoa migogoro ya kukashfiana
baina dhehebu na dhehebu,hali itakayofanya jamii kuzidi kuishi kwa amani na
upendo,huku kamati hiyo ikiwajibika kushirikiana na serikali kutokomeza mauaji
hayo pamoja na matumizi ya madawa ya kulevya kwa vijana.
Awali akimkaribisha mkuu
wa wilaya,Kaimu Sheikh wa wilaya,Sheikh Ramadhani Damka,alisema wilaya ya
Kahama wakazi wake ni wakarimu na wapenda maendeleo,lakini wanakabiliwa na
changamoto kadhaa ambazo viongozi wa serikali wanahitaji kutumia hekima kuzitatua.
Hata hivyo Sheikh Damka
alisema sifa ya wilaya ya Kahama inaharibiwa na baadhi ya maeneo,kunakofanyika
vitendo vya mauaji ya vikongwe na albino kwa imani za kishirikina,ambapo
viongozi wa dini wanajitahidi kusimama imara kuiasa jamii kuepuka matendo hayo
yasiyompendeza Mwenyezi Mungu.
Kwa upande wake Sheikh wa
Mkoa wa Shinyanga,Alhaji Sheikh ismail Habibu Makusanya,alimkumbusha Mkuu huyo
wa wilaya umuhimu wa viongozi wa dini katika suala la kusimamia amani
nchini,kuwa ni mkubwa kutokana kuwa na watu wengi nyuma yao,hivyo ni vyema
serikali ikawapa kipaumbele kila wakati si kwenye kipindi cha shughuli za
kitaifa tu.
Alhaji Sheikh Makusanya
alisema ni vyema serikali ikaondokana na kasumba ya kuona umuhimu wa viongozi
wa dini pindi kunapokuwa na ugeni wa Kitaifa ama yatokeapo majanga,wanastahili
muda wote kupewa kipaumbele na serikali,kwani wanafahamu mengi maovu yenye
athari kwa jamii kwa kuwa wanayoyatenda ni miongoni mwa waumini wao.
Baraza la Idi kimkoa ni
mara ya kwanza kufanyika wilayani Kahama,ambalo lilitanguliwa na sala yake
iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Kahama Muslimu,ambapo
viongozi wa dini waliwaasa waumini waliohudhuria ibada hiyo suala la
upendo,kuvumiliana na kumcha Mwenyezi Mungu.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI