IMEBAINIKA kwamba kupata vilema vya
maisha kutokana na ajali kwa Madereva pikipiki(Bodaboda)wengi hapa nchini,kusababishwa
na kutokuwa kwao makini katika kuzingatia sheria za Usalama barabarani pindi wakiwa
katika shughuli zao za kutafuta riziki.
Sambamba na hilo Madereva hao wa
pikipiki,ndio wanatajwa kuongoza kwa ajali za barabarani,zinazosababisha
kupoteza kwa uhai wao na wateja wao,ama kupata kilema cha maisha.
Hayo yalibainishwa juzi na Mkufunzi
kutoka chuo cha ufundi cha Kingwande cha Jijini Mwanza, Ndege Masara,katika
semina ya siku nne,iliyojumisha madereva pikipiki iliyofanyika Mjini Kahama,chini
ya udhamini wa Mbunge wa Jimbo hilo;Jumanne Kishimba.
Masara alisema kuwa Madereva
pikipiki hao wamekuwa hawapo makini katika shughuli zao wakiwa barabarani hali
ambayo imefanya kuongezeka kwa ajili za Pikipiki na kuwasababishia kuwa na
vilema vya maisha pamoja na abiria wanaowabeba.
Mkufunzi huyo aliendelea kusema,kwa
sasa Bodaboda hao wanapaswa kuwa makini wanapokuwa barabarani ikiwa ni pamoja
na kutambua nini cha kufanya katika kazi yao hiyo ya uendeshaji wa vyombo hivyo
vya moto ili kuweza kupunguza ajali.
Pia aliwataka kutumia mafunzo hayo
ya siku nne wanayoyapata katika kufuata sheria za barabarani hali ambayo
italeta mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kuacha kubeba abiria wawili
wawili katika pikipiki moja,kitendo kilichoelezwa kuwa chanzo kinachosababisha
ajali kwa urahisi.
Hata hivyo,Mkufunzi huyo aliwataka
bodaboda hao,kuwa na utaratibu wa kujiwekea akiba kutokana na kazi hiyo,ikiwa
ni pamoja na kusomesha watoto wao ili kuleta mabadiliko chanya katika familia
wanazotoka,pamoja na watu wanaowategemea.
Kwa upande wake,Koplo Daudi Lugora,kutoka
katika kitengo cha usalama Barabarani Mjini Kahama,aliwataka madereva hao
kuzingatia masomo wanayoyapata kutoka kwa Mkufunzi huyo ikiwa pamoja na
kuwahamasisha wenzao kujitokeza ili kupata mafunzo hayo,yatakayowawezesha
kupata vyeti vitakavyokuwa msingi mkubwa kwao,kupata leseni kwa urahisi.
Koplo Daudi alisisitiza kwa madereva
hao kuacha tabia ya kunywa pombe,wakati wakiendesha Pikipiki ili kuweza
kupunguza ajali ambazo sio lazima, ambazo zinaweza kutokea kutokana na kutumia
vilevi hivyo.
Mafunzo hayo ya Madereva Pikipiki
yalijumuisha washiriki zaidi ya 200,kwa
lengo la kukuza Wajasiliamali wadogowadogo waliopo katika Mji wa Kahama
hususani madereva wa bodaboda.
Kwa upande wake Katibu wa Mbunge wa
Jimbo la Kahama Mjini,Abdul Mpei,akiongea kwa niaba ya Mbunge huyo, aliwaasa Vijana
katika jimbo hilo ni budi wabadilike kwa kufanya kazi kwa kufuata sheria za
nchi,ikiwa ni sambamba na kupata leseni ili waweze kuwa huru katika biashara
zao.