IMEELEZWA kwamba
kuanzishwa kwa vikundi vya vijana katika eneo linalozunguka Migodi kisha
kupatiwa elimu ya ujasiriamali,itasaidia kuondoa migogoro baina ya Mwekezaji na
jamii ambayo itakuwa imepatiwa elimu ya kujikwamua kiuchumi kupitia fursa
mbalimbali za Ujasiriamali.
Hayo yalielezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyang’hwale,
Venance Ngereuya,wakati wa ufungaji mkataba baina ya Mgodi wa Bulyanhulu uliopo
Wilayani Kahama na Shirika lisilo la Kiserikali la Africare,unaogharimu Shilingi
milioni 600.
Mkataba huo huo utakaodumu kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu ni kwa
ajili ya kuunda vikundi vya ujasiliamali kwa vijana waishio kuzunguka migodi huo,utawanufaisha
vijana kutoka vijiji viwili katika
Wilaya za Nyang’hwale mkoani Geita na vingine 12 kutoka Halmashauri ya
Msalala Wilayani Kahama
Ngereuya alisema uanzishwaji wa vikundi hivyo vya vijana kupitia mradi
utakaotekelezwa na Africare,utasaidia kuondoa dhana ya vijana kuwa ajira ni
budi ufanye kazi Mgodini,bali ujasiriamali utaweza kuwakwamua kimaisha kwa
kutumia fursa zitakazowawezesha kufanya biashara na Mwekezaji.
Hata hivyo aliomba uanzishwaji wa vikundi hivyo sambamba na utoaji
elimu,ufanyike kwa umakini mkubwa kwa kulenga vijana stahiki kutoka katika
vijiji husika,vinginevyo tatizo la ajira katika maeneo hayo halitatuliwa pindi
wakinufaika vijana ambao hawana maslahi na vijiji hivyo.
“Kama umakini usipotumika kupata vijana sahihi katika maeneo
hayo,vijiji hivyo havitanufaika na tatizo tutakuwa hatujaliondoa,kwani iwapo
elimu itawafikia vijana wasio na asili ya maeneo husika wataondoka wakinufaika
na mafunzo hayo kwenda kuyatumia walikotoka,”alisema Ngereuya.
Kwa upande wake Meneja Ustawi na Ufanisi wa Mgodi,Elias
Kasitila,alisema mradi huo utakaotekelezwa na Africare umefika kwa wakati
muafaka,kwani utatoa fursa kwa vijana ambao wamehamia katika eneo la Mgodi kwa
lengo la kutafuta ajira,kutambua kuna fursa za kujiajiri na kufanya biashara na
Mgodi na si kutegemea kuajiriwa.
Kasitila alisema mpango huo ambao utatekelezwa kwa ushirikiano wa pande
tatu ambazo ni mgodi wake wa Bulyanhulu, shirika la Africare Tanzania pamoja na
serikali katika Halmashauri hizo mbili za Nyang’hwale na Msalala ambazo zitatoa
wataalamukwa ajili ya ushauri na kusimamia mpango huo.
Kwa upande wake,Kaimu Mkurugenzi wa shirika la Africare Tanzania,
Alfred Kalaghe, alisema kupitia mradi huo wa miradi midogomidogo ya kuboresha
Uchumi,utaanza kutoa mafunzo kwa vijana kabla ya kuunda vikundi
vitakavyowezeshwa mitaji ya kufanya biashara,na watajikita kwenye nyanja mbalimbali
ikiwemo kilimo na ufugaji.
“.... vijana hao tutawawezesha kilimo cha kisasa ambacho kitazalisha
mazao bora yatakayosimama, kwenye masoko na kusaidia kuwainua kiuchumi,na
kuondokana na ndoto za kukimbilia kwenye machimbo kusaka ajira,”alisema
Kalaghe.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI