MKUU mpya wa Wilaya ya Kahama,Fadhili Nkulu,juzi alianza kazi ya wadhifa wake
alioteuliwa na Rais John Pombe Magufuli kufanya kazi wilayani Kahama,kwa
kuwapiga mkwara wakuu wa Idara katika halmashauri zote tatu kwa kuwazuia kuingia
kwenye kikao chake wale ambao walichelewa kufika katika muda uliokuwa umepangwa.
Nkulu aliwaita ofisini
kwake wakuu wa Idara wote katika halmashauri zote tatu za Mji ,Ushetu na Msalala
kwa lengo la kujitambulisha na kufahamiana na walikubaliana kikao hicho
kingefanyika saa mbili asubuhi ofisini kwake,lakini kulingana na mazoea
yaliyojengeka kwa baadhi ya watumishi baadhi yao walifika zaidi ya saa mbili
.
Kufuatia hali hiyo Nkulu
aliwazuia kuingia kwenye kikao hicho wale waliofika zaidi ya saa mbili na
kuwataka wakae nje ya ofisi yake,kwa kuwa makubaliano ya mwaliko huo hayakuwa
kufika zaidi ya saa mbili ingawa Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Anderson
Msumba alinusulika kwenye mkasi huo,baada ya kufika sekunde chache kabla wakati muafaka wa kikao kuanza.
“wewe umefika imezidi
sekunde moja baada ya saa mbili wewe ingia wengine watakao kuja kuanzia sasa
hawataingia kwenye kikao changu watakaa nje kusubili kutokana na kutotekeleza
kufuata ratiba ya vikao “alisema Nkulu ingawa hata baada ya kumaliza kikao chake
na wale waliowahi kufika alitoka nje na kuingia kwenye gari na kuendelea na
ratiba zake zingine .
Hali ya Mkuu huyo wa Wilaya
kuwazuia kuingia kwenye kikao chake wakuu wa Idara waliochelewa kufika
imepongezwa na umoja wa wazee wa Wilaya ya Kahama,ambapo Katibu wake,Paul Ntelya,alisema kasi hiyo ni nzuri ambayo itawafanya wafanyakazi hao kuacha kufanya kazi
kwa mazoea .
Ntelya alimpongeza Mkuu
huyo wa wilaya kwa kasi yake hiyo na kumtaka aendelee kuwa mkali kwenye nidhamu
ya watumishi wa umma ambao wengi wao wanafika kwenye matukio ya kazi zao kwa
muda wanaotaka na si kwa wakati unaotakiwa wengine mpaka hadi ofisini wanafika
wanavyotaka.
“kwa mfano sisi wazee
tulikubaliana kukutana saa nane mchana siku hiyo lakini saa saba na nusu wote
tulikuwa tumeshakusanyika iweje wao wakuu wa Idara wakubaliane kukutana saa
mbili watu wafike saa tatu mkuu huyo yuko sahihi kabisa kuwazuia kuingia
watumishi hao’’alisema Ntelya.
Nkulu ameanza kazi kahama
katika uteuzi mpya wa wakuu wa wilaya uliofanywa hivi karibuni na Rais John
Pombe Magufuli na kabla ya hapo Mkuu wa Wilaya ya Kahama alikuwa Vita Kawawa
aliyeteuliwa mwaka jana wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu na alikuja kushika
nafasi ya Benson Mpesya aliyehamishiwa Wilaya ya Songea kabla ya kusitaafu
nafasi hiyo mwaka huu .