WAKATI Katibu Mkuu wa
Chama cha Wananchi (CUF),Maalim Seif Sharifu Hamad,akimtaka aliyekuwa
Mwenyekiti wa chama hicho,Professa Ibrahim Lipumba,kusubiri hatima ya maombi
yake ya kurejea katika wadhifa aliojiondoa kuamriwa na Baraza Kuu,Koplo mstaafu
wa JWT,Stephen Masanja,ametangaza kugombea nafasi hiyo.
Akiongea na Tanzania
Daima nyumbani kwake,Koplo Masanja,ambaye ni Katibu wa CUF wilaya ya
Kahama,alisema pamoja na kwamba tarehe haijatangazwa ya kufanyika Mkutano mkuu
wa Uchaguzi,lakini anatangaza adhima yake ya kuwania nafasi hiyo kubwa ndani ya
chama.
Koplo Masanja,alisema
ataomba kwa mara ya pili nafasi hiyo baada ya kuthubutu kufanya hivyo kwa mara
ya kwanza katika uchaguzi wa mwaka 2009,akiwa na akina Profesa Abdallah Safari
na Ibrahim Lipumba,na kufanikiwa kushika nafasi ya pili,baada ya kuachwa kwa
kura nyingi na Profesa Lipumba,nae akimuacha kwa kura chache Profesa Safari.
“Nia yangu ya kugombea
ni kutaka kurudisha chama kwa wanachama wilayani na katika Kata na matawi.Kwa
muda mrefu sasa CUF imebaki makao makuu tu,viongozi wanafanya siasa kwa Lap
top,sasa utampataje mwanachama wa Nkasi na Ushetu,kwa Lap Top?”alihoji Koplo
Masanja.
Aliongeza kwa kusema,
“Nikipewa ridhaa ya kuwa Mwenyekiti nitahakikisha nimefika kila wilaya hapa
nchini kwa lengo la kuimarisha chama na kuwapa malengo viongozi wa kila wilaya
kufika katika Kata,na wa Kata kufika kila Kitongoji na Mtaa.”
Koplo Masanja alisema
lengo ni kuirudisha CUF ya mwaka 2000,iliyokuwepo hadi vijijini kinyume na ya
zama hizi ambayo imejikita katika baadhi ya maeneo kwa uchache,hususani
ya mjini,na kumuelezea aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho anayetaka kurejea
katika wadhifa huo kuwa haeleweki.
“Professa Lipumba si
kiongozi wa mapambano,alikitosa chama wakati wa mapambano,leo mapambano
yamekwisha anataka kurejea si kiongozi thabiti,haeleweki na hastahili
kukabidhiwa tena jahazi la CUF,maana anayumba hana msimamo,”alisema Koplo
Masanja.
Hivi karibuni Profesa
Lipumba aliibuka na kudai amemuandikia Katibu wa CUF,Maalim Seif na Baraza Kuu
la Uongozi,kutengua maamuzi yake ya kujiuzuru wadhifa huo,akinukuu Katiba ya
chama chao Ibara ya 117,inayoelekeza namna ya kurejea kwa mwanachama na
kiongozi yeyote aliyeondoka ilimradi hakujivua uanachama.
Hata hivyo Maalim Seif
alitamka hana mamlaka ya kumrejesha bali asubiri maamuzi ya Kikao cha Baraza
Kuu la Uongozi ambacho kitaketi kwa kufuata kalenda ya vikao vya chama.
Tayari baadhi ya
wanachama wa CUF,wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la chama,Twaha
Taslima,ambaye amejinasibu kufanikisha chama kupiga hatua zaidi ya hiyo
iliyofikia,wameonesha nia ya kumrithi Profesa Lipumba katika wadhifa huo.
Mwingine ni Mbunge wa
Liwale,Mohammed Kuchauka,huku kukiwa na tetesi ya Mbunge wa Ukonga,Mwita
Waitara,nae kuwa na nia ya kuwania wadhifa huo.
Koplo Masanja ni
mwanachama mwanzilishi wa CUF,chini ya James Mapalala,ambapo alifanikiwa
kushika nafasi kadhaa za chama,na kabla ya mfumo wa vyama vingi amepata kuwa
Katibu Msaidizi wa UVCCM wilaya ya Kahama mnamo mwaka 1977 hadi 1978,kabla ya
kuajiriwa Jeshini.
Anabainisha kuwahi
kushika nafasi ya katibu wa Shina mara baada ya kuajiriwa Jeshini na kufanya
kazi katika ofisi moja na Rais Mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete katika
chuo cha maafisa wa Jeshi Monduli.