SERIKALI ya awamu ya Tano haitakuwa
na ajizi kumuacha Mkuu wa Mkoa ama Wilaya yeyote kuendelea na wadhifa huo huku
akiwa ameshindwa kutekeleza agizo la kuhakikisha hakuna Mwanafunzi atakayekaa
chini kwa uhaba wa madawati kuanzia Julai Mosi mwaka huu.
Rais John Magufuli alikiwaapisha
Ikulu,Dar Es Salaam, Wakuu wa Mikoa,aliwaagiza kuhakikisha shughuli ya madawati
inakamilika ifikapo Juni 30,mwaka huu.Na agizo lake limetiliwa mkazo na Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George
Simbachawene.
Tangu kutolewa kwa agizo hilo wakuu
wa mikoa na wilaya wamekuwa wakihangaika kulitekeleza huku wengine wakilazimika
kuitisha harambee ili kuomba wananchi wachangie.
Akisisitiza juu ya agizo hilo alipozungumza
baada ya kufungua mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi kuhusu namna ya
kuweka mahusiano mazuri baina ya wawekezaji na wananchi ili kupunguza migogoro
ya ardhi, Simbachawene alisema kila DC na RC ajipime kwa utekelezaji wa agizo
hilo.
Amesema kipimo cha wakuu wa mikoa na
wilaya ni utekelezaji wa agizo la kuhakikisha hakuna mwanafunzi atakayekaa
chini kwa uhaba wa madawati.
Anasema “Mkuu
wa mkoa au wilaya asiyetimiza agizo la kuhakikisha wanafunzi wote wanakaa
kwenye madawati hatoshi, hivyo wanapaswa kujitafakari na kutumia siku zilizobaki
kuhakikisha wanatekeleza.
Alisema zipo wilaya zilizofanikiwa
kutekeleza agizo hilo huku baadhi ya mikoa ikifikisha asilimia 80 na mingine
ikiwa bado kwenye hatua za mwanzo.
Simbachawene alisema Serikali
imeruhusu raslimali za misitu kutumika kwa jili ya kutekeleza agizo hilo na
baadhi ya vibali vimeshatolewa kwa ajili ya uvunaji wa misitu.
“Nitashangaa
kama kutakuwa na mkoa bado unasuasua wakati Serikali imesharuhusu raslimali
zilizopo zitumike kwa ajili ya kutengenezea madawati,”alisema.
Aliongeza kuwa wanatarajia kutoa tathmini
ya hali ya madawati nchi nzima, mwishoni mwa mwezi huu baada ya agizo hilo
kufikia ukomo wake.
Hata hivyo, alisema Rais Magufuli
ndiye atakayetoa agizo la mwisho kwa wale watakaoshindwa kufikisha adhma hiyo.
Kuhusu wawekezaji Simbachawene alisema
wawekezaji wanalazimika kutengeneza uhusiano mzuri baina yao na wananchi ili
kuepuka migogoro.
Alisema Serikali haitahusika iwapo
wananchi watakataa ardhi yao isiwekezwe licha ya kuwapo kwa mikataba na sheria
zilizowaruhusu kuwekeza.
“Hata
kama kuna mikataba na sheria inawaruhusu wawekezaji hawa bado wananchi lazima
washirikishwe ili nao watoe kibali cha kazi hiyo kufanyika. Unadhani
wakiandamana kwa mabango kuzuia eneo lao lisitumike kwa kutoona faida nini
kitafanyika?Jamii ina umuhimu mkubwa kwenye suala hili,”alisema.
Aliwataka wawekezaji hususani kwenye
sekta ya madini na kilimo, kuwashirikisha wananchi ili waridhike juu ya uvunaji
wa raslimali zao jambo ambalo litawaondolea vikwazo.
Hata hivyo alisisitiza kuwa Serikali
inaendelea kupitia mikataba ya madini ili kuhakikisha kuwa inawanufaisha
wananchi kwenye maeneo husika.
“Kitu
pekee ambacho huwa kinawaudhi wananchi ni pale wanapoona raslimali zao
haziwanufaishi, na hata hao wawekezaji wakiondoka huwa wanaacha uharibifu
mkubwa wa mazingira, ndiyo maana Serikali tunalazimika kuwataka wawekezaji
kuhakikisha uhusiano baina yao na wananchi unaimarika,” alisema.
Mtafiti wa Taasisi ya Uongozi, Dk
Godfrey Nyamrunda alisema mdahalo huo umeandaliwa ili kuongeza uelewa baina ya
wawekezaji, Serikali na wananchi kuhusu uwekezaji.
Mtafiti Mkuu wa taasisi hiyo, Dennis
Rweyemamu alisema migogoro ya ardhi isipodhibitiwa inaathiri uwekezaji na hivyo
kupunguza pato la taifa.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI