Tuesday, May 24, 2016

MGOGORO WA MAKAO MAKUU HALMASHAURI YA MSALALA WAMALIZIKA

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO

KITENDAWILI cha Makao Makuu ya Halmashauri ya Msalala wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga,kilichodumu miaka minne huenda kimepata ufumbuzi,baada ya Kaimu mkuu wa mkoa wa Shinyanga John Mongela, kuumaliza huku akidai atawashughulikia watakaopinga maamuzi hayo.

Akitoa maamuzi hayo katika kikao cha pamoja na madiwani wa halmashauri ya msalala  na watendaji ,Kaimu Mkuu huyo wa Mkoa, alidai yametokana na makubaliano yenye maslahi mapana kwa wakazi wa Halmashauri hiyo,ya kambi zilizokuwa zikisigana za Mwenyekiti Halmashauri hiyo,Mibako Mabubu na Mbunge wa Jimbo la Msalala,Ezekiel Maige.

Mongela ambaye pia ni mkuu wa mkoa wa Mwanza alisema kabla ya kikao hicho,Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga pamoja na baadhi ya viongozi wa juu wa Halmashauri hiyo akiwemo mbunge wa jimbo la Msalala, Ezekiel Maige walikaa na kupitisha maamuzi ya kujenga makao hayo katika  Kata ya Ntobo.

“Uamuzi huu umetokana na makubaliano baina ya Mbunge Maige na Mwenyekiti wa Halmashauri,Mabubu,waliokuwa wakivutana kwa kipindi kirefu licha ya serikali kuwa imeishatoa Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya Ujenzi wa Makao Makuu,ole wenu Madiwani na Watendaji wenye tabia za kupiga simu Tamisemi ili kukwamisha maafikiano, nitawashughulikia,”alisema Mongela.

Aidha alitoa siku saba kwa Idara ya Ardhi kukamilisha kupima eneo hilo pamoja na mchoro wake,huku akisisitiza kama mgogoro huo utaibuka upya wataona umuhimu wa kuomba pesa za ujenzi zibadilishiwe matumizi na wizara husika kwa kuelekezwa katika shughuli zingine za maendeleo.

Kabla ya hapo baraza la madiwani wakati halmashauri hiyo ikianzishwa mwaka 2012 lilipitisha makao hayo kujengwa Busangi na tayari serikali kupitia ofisi ya waziri mkuu ilituma wataalamu wake ambao walikubaliana kwa uamuzi huo wakatoa na cheti cha usajili lakini baadae, baadhi ya madiwani walibadili uamuzi na kutaka makao hayo yajengwe Kata ya Segese.

Mabadiliko hayo yalileta mvutano mkubwa serikalini ambapo wakuu wawili wa Mkoa wa Shinyanga Ally Lufunga na Anne Kilango ambao uteuzi wao ulitenguliwa walishindwa kuutatua zaidi ya kuzidisha mpasuko baina  ya makundi yaliyokuwa yakirumbana juu ya sehemu sahihi ya kujenga Makao Makuu hayo.

Akizungumzia maamuzi hayo,Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Mibako Mabubu alisema ni matokeo ya mazungumzo shirikishi yaliyosimamiwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa,kwa kuwakutanisha na Mbunge kujadili tofauti na Wakuu wa Mikoa waliopita,Lufunga na Kilango ambao maamuzi yao yalikuwa ya kibabe,na kudai msimamo wake ulitokana na kusimamia maamuzi ya Madiwani.

Kwa upande wake Maige alisema suala la mvutano huo limemdharirisha sana na kuonekana hafai kwenye jamii,kutokana na baadhi ya madiwani kumtuhumu kuhusika kukwamisha makao hayo kwa kushinikiza kuwa Kata ya Busangi kwa maslahi yake binafsi,jambo ambalo halikuwa kweli hivyo kumalizika kwa mgogoro huo kumemfanya apumue na kuomba washirikiane kuijenga Msalala.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI