Friday, April 15, 2016

ASILIMILIA 71 YA WATANZANIA HAWAFANYI KAZI BALI HUJIKITA KATIKA STAREHE

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO



Utafiti uliofanyika hivi karibuni na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) umebaini kwamba asilimia 71 ya watanzania wanatumia muda mwingi kufanya shughuli zisizokuwa za uzalishaji mali wala tija binafsi kwao na Taifa kwa ujumla.

Akizundua taarifa ya utafiti huo leo jijini Dar es salaam Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,Kazi,Ajira,Vijana na watu wenye ulemavu Mhe. Jenista Mhagama  amesema kuwa idadi hiyo hufanya kazi zisizoleta tija kwao na taifa na muda mwingi huutumia kujihudumia binafsi kwa kulala na starehe nyingine.

Ameeleza kuwa takwimu hizo zinaonesha wazi ni kwa namna gani watanzania wanashindwa kujishughulisha katika kufanya kazi zenye kuwaingizia kipato na badala yake wanatumia muda wao mwingi kufanya shughuli zisizo za uzalishaji hasa kufanya starehe mbalimbali.

 “ Ndugu zangu watanzania unakuta mtu amekaa baa au anacheza “poll table” kuanzia asubuhi mpaka jioni na hujui anafanya kazi gani ya uzalishaji, ndugu zangu tuone aibu basi tujishugulishe tulijenge taifa letu ili kujiletea maendeleo yetu na nchi yetu.”

Aidha, matokeo hayo yamebainisha kuwa asilimia 18.5 ya wananchi wanafanya kazi za uzalishaji na asilimia 10.6 ni wale wanaofanya shughuli za nyumbani zisizo na malipo huku uchambuzi wa kijinsia ukionesha kuwa wanaume asilimia 23.8, wanatumia muda mwingi kwenye shughuli za kiuchumi ikilinganishwa na asilimia 13.5 ya wanawake.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu),Jenista Mhagama,akizindua ripoti ya matokeo ya utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi wa mwaka 2014
Amefafanua kuwa wanawake ambao ni asilimia 16.5 katika utafiti huo wanatumia muda mwingi kufanya kazi za nyumbani zisizo na malipo ikilinganishwa na asilimia 4.4 ya wanaume.

Utafiti huo ulibaini asilimia hiyo ni  ya Watanzania wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 35,ambao  wanatumia muda wao mwingi kwenye shughuli zisizo za uzalishaji mali.

Katika utafiti huo imefahamika Badala ya  kutumia muda huo katika shughuli za uzalishaji mali huutumia  kujihudumia kwenye gesti, baa, kulala na katika shughuli za starehe.

Serikali imesema hali hii inaichelewesha Tanzania kuingia katika kundi la mataifa yenye uchumi wa kati kufikia mwaka 2025.

Bi Ruth Minja, ambaye ni mtakwimu mkuu katika ofisi ya taifa ya takwimu Tanzania, ndiye aliyeongoza utafiti huo wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi kwa mwaka 2014/2015.

Anasema waligundua kuwa watu wenye uwezo wa kufanya kazi walikuwa milioni 25 kutokana na kiashiria cha saa za kufanya kazi kupungua na baadhi ya wafanyakazi kupunguzwa kazi kutokana na utendaji dhaifu.

Aidha Ally Msaki, aliyemuwakilisha Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya kazi,vijana ajira na watu wenye ulemavu , amewaangazia Watanzania walioko kwenye ajira, ambao wanapata kipato ambacho hakitoshelezi kuweza kumudu gharama za maisha.

Amesema nafasi kama hizo za kazi hazina viwango vya ubora na ni kinyume cha maelekezo ya shirika la wafanya kazi duniani ILO.
Ingawa Sera ya taifa ya ajira kwa Taifa la Tanzania kwa mwaka 2008 ilijikita zaidi katika kuongeza fursa za ajira na kufanikiwa katika lengo lake, kuna kasoro kwenye kipengele cha ubora wa ajira


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisa ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa amesema kuwa upatikanaji wa Takwimu hizo utaisaidia Serikali kupata mbinu sahihi za kuondokana na tatizo la ajira nchini kwa kuunganisha nguvu kutoka sekta isiyo rasmi ili kuleta changamoto katika soko la ajira nchini.

Amesema kuwa hii ni mara ya tano Tanzania inafanya utafiti huo na kubainisha kuwa ulianza  mwezi Januari hadi Desemba,  2015 ukitumia sampuli ya Sensa  ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 iliyotumika kupata taarifa sahihi ya takwimu hizo.

Aidha, amebainisha kuwa ili kufanikisha utafiti huo NBS imeshirikiana na wadau mbalimbali ikwemo Wizara ya kazi na Ajira,Shirika la Kazi Duniani (ILO),Benki ya Dunia (WB),Benki ya Maendeleo ya Afrika(ADB) na Asasi zisizo za Kiseikali.

 

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI