RAIS SAMIA APONGEZWA KWA KUTOA FURSA ZA UWEKEZAJI NA AJIRA KWA VIJANA.
Na Ali Lityawi, Kahama.
RAIS wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepongezwa kwa
kuendelea kuweka mazingira yanayowawezesha wawekezaji wazawa kuwekeza, hatua
inayoongeza ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi nchini.
Meneja wa
Kituo cha Mafuta cha Ngara Oil, Nuru Christopher Nzoya, alisema hayo mbele ya
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Michael Mwang'onda, Kahama,
Shinyanga.
Nzoya
alisema fursa zinazotolewa na Serikali zimewezesha wawekezaji wazawa kuanzisha
miradi, hatua inayotarajiwa kutoa ajira kwa vijana wengi wasiokuwa na ajira
nchini.
Alisema
uwekezaji huo utasaidia vijana kujikimu kimaisha, huku ukichangia pia kukuza
uchumi wa Taifa kupitia shughuli za biashara na ongezeko la fursa mbalimbali.
Nzoya
alisema ujenzi wa kituo hicho ulianza Januari saba mwaka huu, na unatarajiwa
kukamilika Oktoba 30, mwaka huu, kwa mujibu wa mipango iliyowekwa.
Alisema
mradi huo unalenga kutekeleza sera ya Serikali ya kuwashirikisha wadau wa ndani
katika uwekezaji wa sekta mbalimbali, kukuza uchumi na kuongeza ajira nchini.
Alibainisha
kuwa kituo hicho kitakapokamilika na kuanza kutoa huduma za mafuta,
kinatarajiwa kutoa ajira kwa watumishi 20 katika Manispaa ya Kahama.
Kwa
mujibu wa Nzoya, mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimu Shilingi milioni
821.5, huku ukiwa na matarajio ya kuongeza shughuli za kiuchumi eneo hilo.
Akizungumza
baada ya kutembelea kituo hicho na kujiridhisha, Mwang'onda alimpongeza
mwekezaji mzawa kwa kuanzisha mradi mkubwa wenye matarajio makubwa ya kuleta
tija eneo husika.
Mwang'onda
aliwashauri viongozi wa Halmashauri zote nchini kuweka mazingira mazuri ya
miundombinu ili kuwawezesha wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza.
Alisema
mazingira rafiki kwa wawekezaji ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Taifa
inayolenga kuwashirikisha wadau katika uwekezaji wa sekta mbalimbali za
biashara nchini.
Aliongeza
kuwa uwekezaji unaochochewa na mazingira mazuri utasaidia kukuza uchumi,
kuongeza ajira kwa vijana na kuwawezesha wananchi kujikimu kimaisha.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI







