Saturday, August 22, 2026

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO

 

KAHAMA YAVUKA LENGO LA USAJILI NeST KWA ASILIMIA 217.

         


Na Ali Lityawi, Kahama

 

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kahama imevuka lengo la kitaifa la usajili wa makundi maalum kwenye Mfumo wa Manunuzi ya Umma kwa njia ya Kielektroniki (NeST), baada ya kusajili vikundi 326 kati ya 150 vilivyolengwa.

 

Kufuatia mafanikio hayo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Mwang’onda, amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu, kwa kusimamia utekelezaji uliofanikisha usajili huo kwa asilimia 217.

 


Mwang’onda alitoa pongezi hizo baada ya kupokea taarifa katika banda la Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), lililopo viwanja vya Stendi Ndogo ya Malori, Kata ya Majengo, wakati wa ziara yake Kahama.

 

Alisema kuvuka zaidi ya mara mbili ya lengo lililowekwa ni ishara ya uongozi bora, hasa katika kuhakikisha vijana, wanawake na makundi mengine maalum yanapata fursa za kunufaika na fedha za serikali kupitia zabuni.

 


Awali, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Kahama, Mbwana Karata, alisema hadi Agosti 15 mwaka huu, vikundi 326 vilikuwa vimesajiliwa, vikijumuisha vikundi vya vijana 173, vya wanawake 150, vya watu wenye ulemavu viwili na wazee kikundi mmoja.

 

Karata alisema halmashauri imetenga zabuni zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 1.9, huku vikundi vinne vikiwa tayari vimetunukiwa zabuni zenye thamani ya Sh milioni 242.45.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI