TATIZO sugu la Maji linaloikabili Kata
ya Mwanase katika Halmashauri ya Msalala,wilayani Kahama,limekuwa chanzo cha
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya
Mwamandi,kusoma kwa saa moja,huku muda
mwingi wakitumia kuchota maji.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari hiyo,iliyopo
katika Kata ya Mwanase,kwa siku hutumia muda huo kusoma masomo,kutokana na muda
mwingi kuutumia kwa ajili ya kupata maji ya kukidhi mahitaji ya shuleni,ambayo
huyachota umbali mrefu.
Diwani wa Kata ya Mwanase ilipo Shule
hiyo ya Sekondari,Samson Paul, alisema hayo juzi katika kikao cha Baraza la
Madiwani wa Halmashauri ya Msalala,kwa kusema tatizo hilo linaathari katika
sekta ya elimu,kutokana na wanafunzi kulazimika kutembea umbali wa kilometa
mbili kwa ajili ya kupata maji kwa matumizi ya shule.
Alisema wanafunzi hao wanakwenda
shuleni kwa ajili ya kuhudhuria masomo yao ya kila siku,lakini Walimu wao
huwaamuru kufanya kazi ya kusomba maji kutoka katika shule ya msingi
Mwanase ambayo ipo umbali wa kilometa mbili,kitendo ambacho husababisha
kuhudhuria masomo kwa saa moja kutokana na foleni wanayoikuta kwenye bomba.
Diwani huyo aliendelea kusema kuwa
mbali na tatizo la maji liliopo katika shule hiyo, pia Shule hiyo inakabiliwa
na upungufu mkubwa wa walimu kwani kuna Walimu watatu tena wa kiume
tu,wanaolazimika kufundisha zaidi ya Wanafunzi 600 katika sekondari hiyo.
Aidha alisema kuwa kutokana na
upungufu huo wa walimu katika Sekondari hiyo kumepunguza hali ya ufaulu kwa
kiasi kikubwa na kuitaka Halmashauri hiyo kuangalia suala hilo kwani hata
kwa mwaka huu kunaweza kukawa na ufaulu mdogo wa Wananfunzi katika sekondari
hiyo
“ …tunaomba tutatuliwe shida ya maji
iliopo katika kata yetu hasa kwa Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Mwamandi
ambao wanakosa Masomo yao kwa muda muafaka,kwani muda mwingi wanapoteza vipindi
vyao katika kusomba maji kwa ajili ya matumizi shule”, alisema Paul.
Hata hivyo Diwani huyo alisema
kutokana na tatizo hilo la maji katika kata hiyo pia kumesababisha Walimu
wanaopangwa kufundisha katika shule hiyo kukimbia huku wachache waliopo kufanya
maamuzi magumu ya kuishi mjini, hali ambayo inachochea ufaulu mdogo kwa
Wanafunzi wa shule hiyo kila mwaka .
Hata hivyo Mhandisi wa Maji katika
Halmashauri hiyo,Cyprian Ndabavunye alisema kuwa Halmashauri imepanga
kupeleka maji katika Kata hiyo katika mwaka ujao wa fedha kutokana na
kutokuwemo katika bajeti ya mwaka 2017/2018.
Amebainisha sababu ni kutokana na mwaka
huu viongozi wa Kata hiyo walichelewa kuwasilisha bajeti yao kwaajili ya
kuingizwa kwenye orodha ya miradi itakayotekelezwa na kuwasihi wananchi wa Kata
hiyo kuwa wavumilivu katika kipindi hiki.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI