KUFUATIA
matukio ya wanyama aina ya Fisi kutishia usalama wa wananchi hususani watoto
wadogo wanaoenda shuleni nyakati za asubuhi katika vijiji,Wilayani
Kahama,Kamati ya
Ulinzi na Usalama wilayani humo imeamua kudhibiti hali hiyo.
Kamati
ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya,imetoa maelekezo kwa Halmashauri za Msalala na
Ushetu sambamba na Mji wa Kahama,kuanza zoezi la kuteketeza wanyama hao,ambao
wamekuwa wakiingia katika makazi ya watu kufanya usumbufu wa kushambulia mifugo
pia binadamu.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala,Simon Berege,ametoa taarifa juu ya kuanza
zoezi hilo wakati akizungumza na wandishi wa Habari hivi karibuni ofisini
kwake baada ya kikao cha kawaida cha baraza la Madiwani wa Halmashauri
hiyo ambacho kililenga kujadili mambo mbalimba mbali ya maendeleo.
Berege
aliwambia wandishi wa Habari kuwa kwa sasa halmashauri hizo mbili, Msalala na
Ushetu zinaendesha zoezi la kuwasaka fisi hao wanaotishia maisha ya wananchi na
kuwaua kwa kutumia bunduki ili kunusuru maisha ya wananchi hao.
“Hawa
fisi wakiingia vijijini wanatishia maisha ya wananchi hasa wanawake na watoto,
lakini fisi hawa wanawaogopa wanaume hivyo kwa ruhusa ya kamati ya ulinzi na
usalama ya Wilaya tumeanzisha oparesheni maalumu ya kuwatokomeza fisi kwa
kuwaua kwa kutumia bunduki na sumu,” Alisema Berege.
Alisema
inashangaza kwa wanyama hao kushambulia watoto na wananwake huku wakionesha
kuwaogopa wanaume,hivyo kuwataka wananchi kutoa ushirikiano juu ya zoezi hilo
na kuwahi kutoa taarifa pindi inapotokea hali ya hatari juu ya fisi wanaozagaa
katika maeneo yao ili iwe njia rahisi ya kupambana nao.
Aliongeza
kuwa siku hiyo wakati akizungumza na wandishi wa Habari ofisini kwake tayari
fisi mmoja aliuawa na watu wa idara ya wanayama pori katika Kata ya chela baada
ya kutaka kutafuna watoto na kutaja idadi ya jumla ya fisi waliouwawa kuwa ni
fisi 14.
Akifafanua
zaidi juu ya idadi ya fisi waliouawa ili kuwanusuru zaidi wananchi kuliwa na
fisi hao Mkurugenzi huyo alisema kuwa katika kikijiji cha Kakola waliuawa
fisi 7 Kata ya Ngaya waliuawa fisi 6 na Kata ya Chela aliuawa fisi mmoja (1)
kulingana na vijiji hivyo kuwa na mabonde pamoja na mapango mengi zoezi hilo
litakuwa endelevu.