IMEELEZWA jitihada za Halmashauri ya
Msalala,wilayani Kahama,kuhamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii
(CHF),zinakwazwa na
kauli mbaya zitolewazo na Wauguzi.
Watumishi hao wa Idara ya
Afya,wamekuwa na lugha zisizo rafiki kwa wanaowahudumia,kiasi cha kuwakatisha
tamaa wagonjwa wanaofika katika vituo vya Afya kwa lengo la kupatiwa matibabu.
Diwani wa viti maalumu Kata ya
Segese,Angela Paul,ameyabainisha hayo katika Kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika
juzi mjini Kahama,kwa kuwataka watumishi wa Idara ya Afya,wajirekebishe na
kuondokana na lugha chafu kwa wagonjwa ili jamii ihamashike kujiunga na CHF.
Diwani huyo alisema kumekuwa na
malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wanaofika katika zahanati na vituo vya
afya,vilivyo Halmashauri ya Msalala, kuwa watumishi wa idara hiyo wamekuwa
wakiwajibu wagonjwa majibu ya kukatisha tamaa pindi wanapoenda kupatiwa huduma
za afya.
“…huu mpango wa CHF,utawawia vigumu
kuenea katika vijiji vyetu pindi lugha chafu kutoka kwa Wauguzi wetu
haitokoma,kwani wamekuwa na vitisho na majibu machafu yanayokatisha tamaa
yanayotolewa na watumishi hao,hivyo jamii kupata hofu kwenda kupata matibabu.”
Alisema Angela.
Angela alidai kuwa tatizo kubwa la
lugha chafu zinazotolewa kwa wagonjwa na watumishi hao ni kutokana na watumishi
hao kufanya kazi kwa mazoea huku asilimia kubwa ya watumishi hao wamedumu
katika vituo vyao vya kazi kwa muda mrefu.
Aidha diwani huyo hakusita kulaumu
mfuko huo wa afya ya jamii(CHF) kwani pamoja na wananchi vijijini kuchangia
mfuko huo lakini changamoto kubwa imekuwa ni kukosekana kwa dawa katika vituo
vya afya pamoja na zahanati zilizopo katika maeneo yao.
Alisema kuwa amekuwa akifanya ziara
nyingi vijijini za kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko huo ambapo wamekuwa
na mwitikio mkubwa lakini changamoto kubwa aliyoiona ni kukosekana kwa dawa
jambo ambalo linawakatisha tamaa wananchi walio wengi kujiunga na mfuko
huo.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya
Msalala,Dr. Hamad Nyembea, aliliambia baraza hilo kuwa upatikanaji wa dawa hivi
sasa ni mzuri kwa kipindi cha miaka mitatu na kuongeza kuwa dawa muhimu
zinapatikana katika vituo vyote kwa asilimia 75.
Akizungumzia kwa kutolewa kwa Lugha
chafu kwa wagonjwa Nyembea alikiri kuwa tatizo hilo lipo na kuongeza kuwa
tatizo hilo linashughulikiwa na mpaka sasa malalamiko mengi yalionyesha
kupungua katika maeneo mengi,huku akibainisha kuwepo kwa mkakati wa kuwabadiri
vituo vya kazi kwa watumishi waliohudumu eneo moja kwa kipindi kirefu .
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Halmashauri hiyo,Simon Berege,aliwaonya watumishi wanaoendelea kutoa lugha
chafu kwa wagonjwa na kuahidi kulitafutia ufumbuzi suala hilo na kudai kuwa
iwapo atabainika mtumishi yoyote wa afya kukutwa na kosa hilo halmashauri
haitasita kumchukulia hatua za kinidhamu.
“Niwaombe wananchi wa Msalala kutosita
kutoa taarifa kwa viongozi,pindi watakapobaini kuna mtumishi wa idara hii bado
anaendelea kutoa lugha chafu kwa wagonjwa,nami sitasita kuchukua hatua kali
dhidi yake kwani tulishaelekezana kupitia vikao vyetu vya utumishi,” Alisema
Berege.