Friday, January 13, 2017

KABELA CITY YA KAHAMA YAZIDI KUCHANJA MBUGA MICHUANO YA TFF.

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO


TIMU ya Soka ya Kabela City ya wilaya ya Kahama,Mkoani Shinyanga,imefanikiwa kusonga mbele katika Michuano ya Kombe ya Shirikisho la Soka Nchini"TFF",baada ya kuisambaratisha timu ya
Murusagamba FC kutoka Mkoa wa Kagera,kwa kipigo cha bao 4 – 0.

Ikicheza mbele ya umati wa mashabiki wake waliofurika katika uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Kahama,Kabela City ilitandaz soka safi na kuonesha dhamira ya kufika mbali kwenye michuano ya kombe la FA maarufu kama kombe la Azam;anaripoti Paschal Malulu.

Timu ya Murusagamba FC ililianza pambano hilo kwa kasi,ambapo walifanya mashambulizi kwenye lango la Kabela City  hali hiyo iliwapa wakati mgumu mashabiki wa timu   mwenyeji kuwa na matumaini ya kuibuka na ushindi.

Hata hivyo Murusagamba FC pamoja na kulisakama goli la Kabela City kwa dakika tisa mfululizo hawakufanikiwa kupata bao,mnamo dakika ya kumi ya mchezo vijana wa Kabela City waliamka na kuanza kujibu mashambulizi kwa kulisakama lango la wapinzani wao.

Vijana wa Kabela City walifanikiwa kupata bao la kuongoza mnamo dakika ya 12 ya mchezo lililofungwa kwa kichwa na Elias Kisusi baada ya kupokea kona maridadi iliyopigwa na Abuu Wakati.

Mnamo Dakika ya 15 Murusagamba FC walipata penati tasa baada ya mchezaji wake kupiga shuti kali na mpira huo nje ya lango.

Katika dakika ya 19 mchezaji Mkiwa Bonzo aliwanyanyua mashabiki wa Kabela City kwa kuandika bao la pili na kuendelea kuwapa wakati mgumu wapinzani wao kusawazisha mabao hayo, hadi mapumziko bao zilikuwa 2 -0.

Kipindi cha pili kilinza kwa timu zote kushambuliana kwa kutengeneza nafasi za kupata bao dakika ya 52 Mkiwa Bonzo akarejea kambani kwa kufunga bao la tatu kwa timu ya Kabela City,kabla ya dakika ya 76,Mkiwa Bonzo tena kupachika bao la nne,na kufanikiwa kupiga tatu za kwake (hat-trick).

Baada ya pambano hilo,Kocha wa timu ya Kabela City,Joshua Maganga alisema ni kazi nzuri vijana wake wamefanya,na wanastahili ushindi kwa kuwa wanacheza kulingana na maelekezo anayowapatia na na kusisitiza wataendelea namazoezi makali ambayo yatawasaidia kufanya vyema katika kombe hilo.

“…sisi kila mechi ni fainali na timu iwe ya wapi hapa nyumbani kutufunga sio rahisi sisi kila anaekuja usoni kichapo tangu ligi ya wilaya hatujawahi kufungwa sisi kufungwa kwetu ni sare mashabiki waendelee kutushangilia tu”.Alisema Maganga.

Kwa upande wake nahodha wa Murusagamba FC,Ibrahimu George alisema kuwa moja ya sababu ya kufungwa kwao ni maamuzi ya mwamuzi wa mchezo huo ambapo alikuwa anatoa lugha ambazo zilichangia kuwatoa mchezoni wachezaji wa timu hiyo.

“ilikuwa mwamuzi nikimfuata kuhusu maamuzi anayotoa anatoa lugha za matusi kweli ilikuwa ni ngumu kwetu kushinda lakini niseme tumekubali matokeo”.Alisema.

Timu ya Kabela city sasa ina subiri ratiba ya mshindi wa mchezo kati ya Jangwani ya mkoani Rukwa dhidi ya Bagamoyo FC ya mkoani Pwani ambapo mchezo huo unataraji kupigwa January 15 ama 16 kwa Kabela City kusafiri kwenda mkoani Pwani ama mkoani Rukwa.

MWISHO.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI