RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania,John Pombe Magufuli,ametumia fursa ya kuhudhuria ibada ya Jumapili,kwa
kutetea maamuzi yake ya kuwatimua baadhi ya watumishi wa umma,wanaokiuka
maadili,kwa lengo la kutaka kuirejesha nchi kwenye mstari.
Rais amesema hayo jana alipozungumza
na waumini kwenye misa ya Jumapili, katika Kanisa Katoliki parokia ya Tokeo la
Bwana Burka jijini Arusha,kwa kusisitiza kumuombea na kumuunga mkono
kukabiliana na watu katili ambao walikuwa wanawaibia Watanzania na
kuwanyonya wanyonge.
Amesema analazimika kuchukua hatua
ya kuwafukuza kazi si kwamba ni katili, bali lengo ni kuwatumikia Watanzania na
kuirejesha nchi kwenye mstari.
Rais huyo aliyejibatiza “mtumbua
majipu”, amesema Tanzania ni taifa tajiri, hakuna sababu ya wananchi
kulalamika kila kona, kwani kuna ardhi ya kutosha, madini ya kila aina, wanyama
wa aina mbalimbali ambao baadhi wameanza hadi kupelekwa nje.
"Ninapochukua hatua nataka kuweka
Tanzania iliyonyooka, mimi tayari nimesema nimejitoa sadaka kwa watanzania hasa
wanyonge," alisema.