WATANZANIA wameaswa
kuwekeza na kurithisha vijana wao elimu,kwakuwa ndiyo mirathi bora isiyoleta
utengano katika familia na itakayosaidia kutokomeza mauaji potofu ya imani ya kishirikina
sambamba na kuleta chachu ya maendeleo itakayosaidia kukuza uchumi wa nchi.
Hayo yalielezwa na Sheikh
wa wilaya ya Kahama {BAKWATA},Sheikh Omari Damka,katika muendelezo wa
kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad S.A.W yaliyofanyika Kata ya Isaka
katika Halmashauri ya Msalala,ambapo alisema mirathi bora ya kuwaachia watoto
ni elimu.
SHEIKH Omari Damka. |
Sheikh Damka alisema wazazi
wanastahili kuwekeza kwa nguvu katika suala la elimu kwa vijana wao ili kuondoa
migogoro ya kugombea mali pindi wazazi hao wanapofariki kwakuwa kila kijana
atakuwa tayari ana mirathi yake ambayo ni elimu itakayomsaidia kukabiliana na
changamoto za maisha.
Alisema ni vyema wazazi
wajinyime kusudi vijana wao wapate elimu,ambayo itakuwa msingi wa maisha yao
sambamba na kusaidia kutokomeza mauaji ya vikongwe yatokanayo na imani za
kishirikina pia mauaji ndani ya familia yatokanayo na kugombea mirathi.
KIJANA Shafii Zubeiry akionesha umahiri katika kusoma Hadithi. |
“Katika umri huu nilionao
sijapata kusikia familia zimeuana sababu ya elimu bali ni kwa ajili ya mashamba
na mali,hivyo mkiwarithisha elimu itakuwa bora,ni vyema mzazi ufirisike kwa
kuwekeza katika elimu kwa kijana wako kuliko kufariki na kuacha mali
zitakazosababisha uhasama wa familia,”alisema Sheikh Damka.
WATOTO Soud Haruna na Mwajuma Khudhaifa wakitoa maelekezo jinsi ya kuswali kwa ufasaha. |
Kwa upande wake Diwani wa
Kata ya Isaka,Dkt.Gerald Mwanzia,aliziomba taasisi za dini kujenga mkakati wa
kielimu na kuandaa miundo mbinu iliyo rafiki kwa vijana ili kusaidia lengo alilokusudia
Rais John Magufuli kutoa elimu bure ambayo itakuwa ina kiwango bora.
WASICHANA Ashura Juma na Maisala Mohammed Kibabi wakitoa mawaidha. |
Aidha aliwakumbusha wazazi
nao kuwajibika katika suala la elimu ili kuhakikisha vijana wanafanya vyema
katika masomo yao hatua itakayosaidia kuondoa umaskini katika familia zao na
taifa kwa ujumla kutokana na kuwa na vijana walioelimika hivyo kuwaomba kuwa
tayari kushiriki katika kuimarisha miundo mbinu ya shule.
MKUU wa Kituo cha Polisi Isaka,Mkaguzi Richard Kapongo. |
Nae Mkuu wa Kituo cha
Polisi katika mji mdogo wa Isaka,Mkaguzi wa Polisi,Richard Kapongo,alisisitiza
wazazi kuwapatia vijana wao elimu na kuwalea katika misingi ya dini ambayo
ndiyo malezi bora jambo litakalosaidia kuondoa uhalifu kwa kuwa watakuwa na
maadili mema yatakayowasaidia kuepuka vitendo viovu.
PICHA ZAIDI ZA KWENYE MAULIDI HAYO;