HOFU imewatawala baadhi ya wazazi
waliojifungua wodi ya wazazi katika hospitali ya Mount Meru ambayo ni hospitali
ya Mkoa wa Arusha,baada ya mtoto mchanga wa siku tano kuibiwa wodini katika
mazingira ya kutatanisha.
Akisimulia tukio hilo,kwa
huzuni, mama mzazi wa mtoto huyo, Sinyari Lucas ambaye ni mkazi wa Simanjiro
mkoani Manyara, alisema lilitokea usiku wa kuamkia jana,huku kutwa nzima akiwa
na mtoto wake kabla ya kuingia usiku na kupitiwa na usingizi..
Aidha Lucas Ngaraa ambaye ni baba wa
mtoto aliyeibiwa,alishangazwa kutokea kwa tukio hilo,huku akihoji limemudu vipi
kufanikiwa ilhali hospitali hiyo ina ulinzi wa kutosha.
Baadhi ya wazazi waliokuwapo kwenye
wodi hiyo, walisema muda wote mzazi huyo alikuwa amelala kitandani na mtoto
wake, lakini usiku walishangaa kumsikia anapiga kelele.
Waliomba
serikali iingilie kati suala hilo ambalo limezusha hofu miongoni mwao wakihofia
juu ya usalama wa watoto wao, kwa madai ni budi jitihada zinafanyika za kuhakikisha
kichanga hicho kinapatikana na kurejeshwa kwa mzazi wake,huku ulinzi
ukiimarishwa kwa ajili ya watoto wao.
Mganga Mkuu Mfawidhi wa
Hospitali hiyo, Dk Jackline Urio alikiri kuwapo kwa tukio hilo na kwamba,
uongozi umelipokea kwa mshtuko mkubwa na unalifanyia kazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Arusha, Liberatus Sabas alisema wamepokea taarifa hizo na tayari ameagiza
maofisa kwenda kufuatilia tukio hilo kwa kina.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI