SAKATA la wananchi wa
Manispaa ya Dodoma kuvamia kitongoji cha Bwibwi Kijiji cha Iyungo,na kujigawia
viwanja kiholela katika eneo hilo lililotengwa na Mamlaka ya Ustawishaji Makao
Makuu (CDA)kwa ajili ya uwekezaji mkubwa limezidi kuchukua sura mpya.
Sakata hilo linazidi
kuchukua sura mpya kutokana na idadi kubwa ya watu kujitokeza eneo hilo,wakidai
ni urithi wa historia yao tangu mwaka 1872 huku wakiapa kupigania eneo hilo kwa
gharama yoyote.
Akizungumza na mamia ya
watu waliojitokeza katika eneo hilo,Chifu wa kabila la Wagogo,Lazaro Machuma Chihoma,alisema
wameamua kung’ang’ania katika eneo hilo kwakuwa ndio sehemu pekee iliyosalia ya
historia ya kabila hilo.
CHIFU wa Wagogo. |
Chifu Chihoma alisema kwa
kutambua umuhimu huo ndio maana hawako tayari kulipoteza kwani pindi likiachwa
na kutumika kwa matumizi mengine kumbukumbu,mila,tamaduni na desturi zitatoweka
kwa vizazi vijavyo.
“Hakuna kitu kinanikera
kama jina la mkoa wa Dodoma,kuja kupotea wakati ni tembo walizama kwenye
kisima,kipo Shule ya Saint John kikuyu,ndio walisababisha ikaitwa Dodoma,kwasababu
hawakuwashirikisha wenyeji wa Dodoma wakati wanafanya vipimo vyao,ndio maana
historia nyingi wanazipoteza,”alisema Chifu Chihoma.
Hivyo aliomba CDA katika
maeneo ambayo hayajapimwa pindi watakapotaka kufanya zoezi hilo ni vyema
wakawashirikisha wananchi wenyeji wa maeneo hayo ili kuepuka mgogoro unaoweza
kutokea kama uliopo eneo hilo.
Aidha baadhi ya wananchi
waliojitokeza katika eneo hilo walimuomba Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya
Makazi,Wiliam Lukuvi,kuingilia kati mgogoro huo wakidai CDA wametumia mabavu
kwani walikuwa wakitumia eneo hilo hadi mwaka 2013,kabla ya Mamlaka hiyo kuvamia
eneo hilo.
Walidai baada ya CDA
kuvamia eneo hilo,ilivunja nyumba zilizokuwa zikitumika kwa masuala ya
kimila,na mnara wa kumbu kumbu ya kuangamia kwa wenzao 29,mnamo mwaka 1872.
Hata hivyo Mkurugenzi wa
Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu,alisisitiza kuwa eneo hilo wanalimiki tangu
mwaka 1978,baada ya kukabidhiwa na Serikali na kulifanya kuwa hifadhi ya msitu
kabla ya mwaka 2010,kuligeuza kuwa la uwekezaji mkubwa.
Hivyo aliwataka wananchi
hao kutotumia fursa ya urithi wa asili kukwamisha mipango ya maendeleo na
kuwataka kuondoka katika eneo hilo kabla sheria haijachukua mkondo wake,na
pindi wakidhani kuna haki zimekiukwa ni vyema wakaenda mahakamani.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI