Sunday, March 27, 2016

BARAZA LA MADIWANI HANANG LAMKATAA MKURUGENZI WAO

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO



BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Hanang,mkoani Manyara,limemkataa,Mkurugenzi wake Mtendaji,Felix Mabula,kwa kutokuwa na imani nae na kuwasimamisha kazi watumishi wanne kwa madai ya tuhuma za ubadhirifu wa fedha zaidi ya Shilingi Milioni 280.

Katika kikao chao maalumu,kilichohusisha madiwani wa CCM na wa upinzani, kwa kauli moja kilichukua maamuzi ya kumkataza kushiriki shughuli zote za Halmashauri hiyo,Mkurugenzi huyo Mtendaji huku ikiwasimamisha kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha ambazo zilikuwa za halmashauri na uchaguzi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang,Geogry Bajuta,alisema wamechukua maamuzi hayo kutokana na ripoti ya mkaguzi wa ndani wa Halmashauri hiyo,ambapo Baraza limetoa mapendekezo kwa mamlaka husika kuwa Mkurugenzi huyo mtendaji asimamishwe kazi ili kupisha uchunguzi.

Aliwataja watumishi wanaosimamishwa kazi sambamba na Mkurugenzi huyo kupisha uchunguzi kuwa ni Mweka hazina wa Halmshauri hiyo;Mazengo Matonya,Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo;Hamisi Katimba,Mhasibu bi Wellu Sambalu na mtu wa malipo Marceli Siima.

“Tumeonewa vya kutosha,Hanang imekuwa shamba la bibi,kila mtu anaingilia huku anachukua sasa na DC nafikiri ana mlango wake wa kuchukua,haiwezekani kwamba yeye anamuunga mkono Mfisadi,wakati Madiwani wamesema hawana imani tena na Mkurugenzi Mtendaji,”alisema Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang.

Kauli hiyo ilikuja baada ya kutokea marumbano baina yao na Mkuu wa Wilaya ya Hanang,Thobias Mwilapya,ambaye hakuafikiana na maamuzi hayo kwa madai kwamba kikao hicho kilikuwa batili,huku akitaka kutoa salamu za wilaya hatua iliyomlazimu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo amuamuru aketi naye kutokuwa tayari kutii amri hiyo.

Baada ya marumbano makali ambapo Madiwani kwa pamoja waliungana kumsakama Mkuu huyo wa wilaya kwa madai anampendelea Mkurugenzi,ilimlazimu kiongozi huyo wa serikali atoke nje ya ukumbi wa mkutano na kuacha madiwani wakisisitiza maazimio yao ya kuwasimamisha vigogo hao wa Halmashauri.

Aidha madiwani hao walishangazwa kwa kitendo cha Mkuu huyo wa wilaya kuonesha nia ya kumkumbatia Mkurugenzi ilhali anafahamu fika uwepo ubadhirifu wa fedha za Halmashauri hiyo,hivyo kuafikiana kuandika barua kwenda ofisi ya Rais TAMISEMI,kueleza juu ya maamuzi yao hayo.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI