MAHAKAMA
kuu Kanda ya Shinyanga inyaosikiliza kesi ya Kupinga Matokeo ya Uchaguzi wa Mkuu
wa Ubunge,Jimbo la Kahama Mjini, uliofanyika Oktoba, 25,mwaka jana;na
kufunguliwa na aliyekuwa Mgombea Ubunge wa Chadema,James Lembeli,dhidi ya
Mbunge Jumanne Kishimba{CCM}, inatarajia kutoa hukumu hiyo wiki ijayo,Machi 31.
Tamko hilo la kutolewa kwa
hukumu hiyo katika tarehe hiyo ambayo itakuwa ni siku ya Alhamis
ijayo,ilitolewa na Jaji wa Mahakama hiyo,Moses Mzuna,wakati wa hitimisho la
kuwasilisha hoja za mwenendo wa kesi hiyo,zilizowasilishwa na mawakili wa pande
zote mbili, baada ya kufungwa kwa
ushahidi wa pande zote mbili.
MBUNGE wa Jimbo la Kahama,anayelalamikiwa;Jumanne Kishimba. |
Katika mwenendo wa shitaka
hilo linalosikilizwa katika mahakama mjini Kahama, Jaji Mzuna,alitoa tarehe
hiyo ya hukumu baada ya Mawakili wa pande zote mbili kuwasilisha mwenendo wa
kesi hiyo tangu ilipofunguliwa hadi kufungwa kwa ushahidi.
Wakili
Mpale Mpoki akiwasilisha hoja kwa niaba ya Mlalamikaji Lembeli, aliiomba Mahakama Kuu kuukubali
ushahidi wote uliotolewa na mashahidi wao; kwa kuwa umekidhi masharti ya
kisheria katika uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi.
Hoja ya Mpoki ilifuatia madai
ya Wakili wa Utetezi, Anthony Nansimire anayemwakilisha Jumanne Kishimba na
wakili wa Serikali Castus Ndamugoba; walioiomba mahakama kutupilia mbali shauri
hilo kwa kuwa ushahidi ulioletwa mahakamani hapo,unaacha mashaka na siyo wa
kuaminika.
Nansimire na Ndamugoba walisema
Ushahidi uliotolewa na Lembeli, Asha Bushesha, Secilia Gregory na Michael
Magimbo haushabihiani; na kwamba wote hawakumtaja Kishimba kuonekana akigawa
viberiti, madaftari na masufuria na kwamba sehemu kubwa ni wa kuambiwa.
Walieleza, Mashahidi muda
wote wakitoa ushahidi wao mahakamani hapo, walikuwa
wakibadilishabadilisha maneno huku wakimtaja Ezra Machogu kuhusika na kugawa
rushwa; maneno yasiyomhusisha Kishimba na matukio hayo hali inayoonyesha kwamba
ushahidi wao ni wa kutunga; hivyo siyo wa kuaminika.
Akijibu hoja hiyo Mpoki alisema,
Mashahidi wote waliotajwa wamemuongelea Meneja Kampeni wa Kishimba; Ezra
Machogu kugawa rushwa au zawadi kwa tafsiri ingine, ambapo mwenyewe aliithibitishia mahakama alikuwa
meneja kampeni mkuu wa CCM jimboni humo.
Awali Nansimire na
Ndamugoba walisema hakuna ushahidi ulioonyesha uhusiano wa Ezra na Kishimba;
hatua iliyoelezwa na Mpoki kwamba ni kutaka kuichanganya mahakama, kutokana na
aliyetajwa kuthibitisha kwamba alikuwa akiwauza kwa ujumla wagombea wa CCM
jimboni humo wa ngazi za Urais, ubunge
na Udiwani.
Katika upande mwingine
Mpoki alisema, pamoja na madai ya upande wa utetezi kuwaapisha wasimamizi 17
waliodaiwa kuukana unachama wa CCM kati ya Oktoba 21-23,2015, kipindi hicho
hakikutoa fursa kwa wananchi kupinga uteuzi huo kama Andrew Feruzi
alivyoshuhudia.
Mpoki alisema, hata Msimamizi
wa Uchaguzi katika Jimbo la Kahama Mjini, Anderson Msumba, akitoa ushahidi wake
aliimbia mahakama kuwa bado ni mwanachama wa CCM na hivyo kiapo chake cha
kuukana uanachama ni uongo; na kwamba maamuzi yake aliyotoa kwenye uchaguzi ni
Batili.
Kuhusu kukamatwa na polisi
wanachama 11 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo-CHADEMA katika hotel ya
Golden Rock Oktoba 25,2015; na wengine watano katika kata ya Ngogwa, Mpoki alisema,
ulikuwa wa kibaguzi na ulilenga kuwatia
hofu wana-CHADEMA.
Mapema akiwasilisha hoja Wakili
Ndamugoba aliiomba mahakama kuzingatia kwamba kuachiwa huru kwa mtuhumiwa
mahakamani hakuoneshi kwamba polisi walimkamata kimakosa; hivyo watu hao
walikamatwa kwa kushukiwa, kitu ambacho kwa polisi kipo kisheria.
Katika usikilizaji wa kesi hiyo ambayo huenda
ikawa hukumu ya kwanza kutolewa kwenye kesi za Uchaguzi,umati mkubwa wa watu
ulikuwa ukifurika kila siku mahakamani huku ukitawaliwa na tambo za ushindi kwa
kila upande,hasa kutokana na ushahidi uliokuwa ukiwasilishwa na kila upande.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI