Saturday, March 26, 2016

KILANGO AIBEBA AHADI ALIYOITOA KIKWETE KWA WAHANGA

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO

IMEBAINISHWA kwamba kutotekelezeka kwa ahadi  ya kujengwa nyumba 342 za wahanga wa Kata ya Mwakata wilayani Kahama,aliyotoa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete,ilitokana na mikakati ya serikali kubaki madarakani katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25,2015,na kwamba ujenzi huo utatekelezwa hivi karibuni.
 
Hayo yalibainishwa na Mkuu mpya wa Mkoa wa Shinyanga Anne Kilango katika ziara yake ya kwanza tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo,na kuamua kutembelea waathirika wa mvua ya mawe wa Mwakata Wilayani Kahama na kuahidi ahadi ya serikali ya awamu ya nne ya kujenga nyumba 342 itatekelezwa.
 
Kilango aliyeteuliwa katika uteuzi mpya wa Rais John Magufuli na kuanza kazi rasmi Mkoani Shinyanga Machi 21 mwaka huu,alisema ahadi hiyo ilichelewa kutekelezeka kutokana serikali ya awamu ambayo ilikuwa ya CCM kuwa katika mikakati ya kuhakikisha inaendelea kushika dola.
 
“Naomba mniamini suala hili nitalishughulikia kwa nguvu na litakamilika,mtambue lilichelewa kutokana na mwaka jana kuwa wa uchaguzi,kwakuwa  ahadi hiyo kuahidiwa na serikali ya awamu ya nne iliyokuwa ya Chama Cha Mapinduzi ambacho mpaka sasa kinaendelea kutawala hivyo ahadi yake hiyo serikali ya awamu ya tano itaitekeleza kwani sasa ni muda muafaka,”alisema Kilango.
 
 Awali akifungua mkutano huo wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mwakata,Diwani wa Kata ya Mwakata,Ibrahim Masanja,alimweleza Mkuu wa Mkoa huyo kuwa uchumi katika eneo hilo umedumaa kutokana na  wananchi kutokuwa na makazi imara na kusababisha waishi maisha magumu huku wengi wao   wakilala maeneo hatarishi.
 
Masanja alisema ahadi ya ujenzi huo iliwafanya wengi wao kutojenga nyumba za kudumu kwa kusubiri kujengewa kama walivyoahidiwa ambao kwa sasa wanaishi kwa ndugu zao kwa kubanana,na baadhi wakilala nje na kuchanganyikana na mifugo hivyo kuhatarisha afya zao,hivyo kuitaka serikali   kuangalia watu hao kama walivyoahidi.
 
Hata hivyo katika eneo hilo tangu maafa hayo yatokee huku Rais Mstaafu kuahadi ahadi hiyo Kikwete,kuna jitihada mbalimbali zilizofanywa na wadau ikiwemo kampuni ya Acacia kupitia mgodi wake wa Buzwagi iliyojenga nyumba za mfano tatu kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 70 ambayo serikali ilisema ingejenga nyumba hizo kwa mfano huo
 
Pamoja na kampuni hiyo ya Acacia kujenga nyumba hizo serikali ilisema nyumba hizi zitakuwa na gharama kubwa hivyo Halmashauri ya Msalala ilijenga nyumba zingine za mfano ndogo zaidi mbili zenye thamani ya shilingi zaidi ya milioni 14 lakini hata hivyo pamoja na gharama kupungua kutoka milioni 70 mpaka sasa hakuna utekelezaji uliofanyika wa kuwakamilishia wananchi hao nyumba.
 
Nae Mkuu wa Wilaya ya  Kahama,  Vitta Kawawa, aliwakumbusha wananchi hao jitihada za serikali ilizozifanya kukabiliana na majanga waliyoyapata na kuwataka kuwa ni wenye shukrani huku akisisitiza kuwa suala lao litakamilika kutokana na mkuu wa mkoa huyo kumfahamu ni mchapakazi na mfuatiliaji kwa kina kuhakikisha kero za wananchi zinatatuliwa.
 
Wananchi hao mwezi machi 4 mwaka jana walikumbwa na mafuliko ya mvua kubwa ya mawe iliyosababisha watu 47 kupoteza maisha yao na wengine mia 900 kutosa mahala pa kuishi kutokana na nyumba zao 403 kubomolewa na mvua hiyo ingawa baada ya tathimini zilibainika nyumba 342 kuonekana haziwezi kukarabatiwa tena zinahitaji kujengwa upya.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI