SERIKALI imetoa karipio kwa wananchi
wavivu,ambao wameshindwa kujituma kufanya kazi,kwa kuwaeleza chakula cha
misaada
pindi kikiingizwa katika maeneo yao kwa madai ya kuwepo upungufu wa
chakula,hakitawahusu.
Imewataka Watanzania wajitume katika
kujipatia ridhiki halali,na kuepuka na kulia maisha magumu ilhali wamebweteka
pasipo kujishughulisha na shughuli halali japo za kujiajiri ili kujiingizia
kipato.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amesema kamwe Serikali haitagawa
chakula kwa wananchi wavivu ambao hawataki kufanya kazi na kusubiri chakula
kutoka Serikalini.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassana ametoa kauli hiyo wakati akihutubia mamia
ya wananchi wa Manispaa ya Musoma katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye
uwanja wa Mukendo mjini Musoma.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan
amesisitiza kuwa Serikali itapeleka chakula kwa wananchi ambao mazao yao
yaliharibiwa kwa mvua au yalikauka kwa ukame au kwa maafa mengine na sio
kwa wananchi wanaokaa vijiweni mchana kutwa bila kufanya kazi wakisubiri neema
ya chakula kutoka kwa Serikali.
Amewahimiza wananchi kote nchini
kuendelea kufanya kwa bidii ikiwemo shughuli za kilimo na pindi wanapovuka
wajiwekee akiba na waache tabia ya kuuza mazao yote wanayovuka ili kukabiliana
na tatizo la uhaba wa chakula kwenye familia zao.
Makamu wa Rais pia amewataka viongozi
wa mkoa wa Mara washirikiane na wananchi katika kuwaelemisha mbinu bora za
kilimo ili waweze kupata mazao mengi ikilinganishwa na hali ilivyo kwa sasa.
Kuhusu tatizo la uvuvi haramu, Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameziagiza
Kamati za Ulinzi na Usalama kufanya misako ya hali na mali katika kupambana na
tatizo hilo ambalo limechangia kupunguza samaki katika maeneo mbalimbali
nchini.
Ametoa mfano kwa mkoa wa Mara kuwa
ulikuwa na viwanda Vinne vya kuchakata samaki lakini kutokana na shughuli za
uvuvi haramu na wa kutumia sumu umepelekea viwanda Vitatu kukosa malighafi hiyo
na kusitisha uzalishaji.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan
amesema jambo hilo ni baya kwa sababu limeikosesha Serikali mapato na
kusababisha wananchi wakose ajira kutoka kwenye viwanda hivyo jitihada za
makusudi lazima zifanyike katika kukomesha uvuvi haramu katika maeneo
mbalimbali nchini hasa katika Ziwa Victoria.
Aidha, Makamu wa Rais ameeleza
kufurahishwa na kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji wa Musoma ambao
umetekelezwa na Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ufaransa na kusema
kuwa mradi huo utaondoa tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa
wananchi wa wilaya ya Musoma.
Amewataka wananchi wa Manispaa ya
Musoma kuulinda na kuutunza mradi huo ili uweze kudumu kwa miaka mingi kwa
ajili ya kuhudumia wananchi wa Manispaa hiyo.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mara Dakta
Charles Mlingwa amewahimiza wananchi wa mkoa wa Mara kuweka itikadi zao kando
na washirikiane katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani
humo.