Friday, June 2, 2017

RAIS MAGUFULI AWASHUKIA WATUMISHI WA SERIKALI KUHUSU MAPATO

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO



RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli,amewataka watumishi wa Serikali kuwa wabunifu kwa
kuibua vyanzo vya mapato vitakavyokuwa msaada wa kulifanya Taifa lisonge mbele Kimaendeleo.

Wameelezwa ni vyema wakaondokana na tabia iliyoota mizizi miongoni mwao ya kuwaza  mambo makubwa ambayo hushindwa kuyatimiza,huku wakikosa ubunifu uliotukuka unaokuwa msaada wa kuliingizia pato Taifa.

Rais Magufuli alisema hayo wakati akizindua Mfumo wa serikali wa ukusanyaji kodi kwa njia ya Kieletroniki,ambapo amewaeleza kinaga ubaga baadhi ya  watumishi wa Serikali wamekuwa wakiwaza mambo makubwa ambayo wanashindwa hata kuyatimiza.

Amesema kuwa watumishi wengi wamekuwa si wabunifu katika kuangalia vyanzo vya mapato ambavyo vinaweza kusaidia serikali kuingiza pesa nyingi lakini wao wamekuwa wakiwaza kuongeza bei ya pombe tu na kuacha vitu vingine ambavyo vingeweza kuongeza mapato kwa serikali kwa njia nyingine nzuri.

Ameshangazwa kuona wanahangaika na Machinga,katika utaratibu ambao hauna tija kwa Serikali na wahusika wenyewe,ambao wamekuwa wakikimbizana nao mitaani.

“…. wakati tungeweza kutengeneza vitambulisho vya wamachinga na kila kimoja tukauza labda elfu kumi, Machinga akinunua kitambulisho hicho anatambulika na serikali na kinaeleza kuwa anapaswa kuwa wapi, je, ni shilingi ngapi tungezipata hapo kwa idadi wa wamachinga waliopo nchi nzima?”Anahoji.

Anaongeza kusema, “Lakini watu wetu wao wanawaza kuongeza bei ya pombe tu, yaani tuna watu wa uchumi wengi lakini sijui hata wanafikiria nini "

Mbali na hilo Rais Magufuli alisema hata tabia ya watu kukwepa kulipa kodi inasababishwa na mipango mibovu akitolea mfano kuwekwa bei juu ya kodi ya majengo jambo ambalo linafanya watu wengine kushindwa kulipa kodi hiyo na serikali kupoteza mapato.

Anazidi kuhoji"Watu wetu hawa hata kwenye kodi ya majengo unakuta wameweka mtu alipe milioni mbili sasa hizo pesa wananchi wanazipata wapi?

“ Ndiyo maana wanakwepa kodi sababu hawana pesa hizo lakini kama wangeweka labda elfu kumi, ishirini mpaka hamsini halafu wenye maghorofa labda laki mbili ungeona kila mtu angekimbilia yeye mwenyewe kulipa kodi, kwa nyumba zote zilizopo Tanzania tungepata shilingi ngapi?”

Rais Magufuli anasisitiza kuwa kuweka pesa kubwa,huku ikishindikana kuzipata inatokana na mipango mibovu,yenye kuwakandamiza wenye vipato duni na kuwa kigezo cha kushindwa kulipa kodi hizo.

Katika hatua ya mwisho Rais Magufuli aliyaomba makampuni ya simu nchini yawe mfano wa kuigwa na ikiwezekana yawe ya kwanza kabisa kujiunga katika mfumo huu mpya wa ukusanyaji wa kodi kwa njia ya kieletroniki kwani mfumo huu una manufaa kwa wawekezaji na Watanzania kwa ujumla.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI