Friday, June 2, 2017

BEI YA PAMBA KUWAREJESHA WAKULIMA WALIOASI ZAO HILO.

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO




MDORORO wa uzalishaji zao la Pamba,uliodumu kwa kipindi cha takribani miaka zaidi ya Ishirini,huenda ukawa umepata muarobaini
katika Awamu hii ya Serikali ya Awamu ya Tano,inayoongozwa na Rais John Pombe Joseph Magufuli.

Jitihada zilizoanza kufanywa kwa kuangalia ongezeko la bei ya Pamba iliyotangazwa,kabla kwa kuanza kwa msimu wa ununuzi wa zao hilo,imeelezwa huenda ikasababisha ushawishi mkubwa kwa wakulima walioliasi kurejea kulima.

Mkulima wa zao hilo,Juma Makashi,kutoka Kata ya Idahina katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama,wakulima waliokuwa wakilima zao hilo walilikimbia na kuhamia katika kilimo cha mazao mengine kutokana na mauzo yake kutokuwa na tija kwa mkulima.

Mkulima huyo alidai bei hiyo ya Shilingi 1100,ni faraja kubwa kwa wakulima wa zao hilo,kwakuwa itawapa fursa ya pato lake kufanya shughuli zingine za kimaendeleo,tofauti na miaka ya nyuma ambapo haikukidhi hata gharama za uendeshaji.

Makashi alisema kutokana na Serikali kuona umuhimu wa kuongeza bei ya zao hilo hivi karibuni,itawezesha kuhamasisha wakulima ambao walilikimbia zao hilo kurejea kulilima katika msimu ujao wa kilimo.

Hata hivyo Chama cha Wakulima wa Pamba Tanzania TACOGA tawi la wilaya ya Kahama,kupitia Kaimu Katibu Mtendaji wake,Paul Ntelya,kiliwaasa wanunuzi wa zao hilo kufika kwa wakati kwa wakulima kufanya biashara hiyo,hatua itakayosaidia kutoharibika kwa zao hilo.

“…mkulima akinunuliwa zao lake na kupata malipo yake kwa wakati,itamjengea hamasa ya kufanya maandalizi kwa msimu unaofuata,kwa kuweka malengo ya kukuza kilimo chake,pia kuwa sababu ya kuwavutia wengine kuamua kulima pamba.”Alisema Ntelya.

Aidha Tacoga iliwaasa wakulima kuwa waaminifu katika zoezi zima la uuzaji zao hilo la Pamba,kwa kuwataka kutotumia mifuko ya sandarusi kufungia zao,kwakuwa imekuwa chanzo cha kulichafua na badala yake watumie nguo za khanga,vitenge ama mifuko ya pamba,kama vifungashio.

Ntelya aliwatoa hofu wakulima wa zao hilo kuwa katika msimu huu hakutokuwepo udanganyifu katika mizani,kutokana na Bodi ya pamba,kuandaa ukaguzi utakaoambatana na Mhakama inayotembea,ambapo Mnunuzi atayebainika kumuibia Mkulima atahukumiwa papo hapo.

Hata hivyo aliwaomba wakulima wasiwe waoga kutoa taarifa katika vyombo vinavyohusika pindi wakiona wanafanyiwa dhuruma katika mauzo yao.

Msimu wa zao la Pamba unatarajiwa kufunguliwa Juni 5,mwaka huu katika Kijiji cha Mwabusalu wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu,huku kukiwa na ongezeko la Shilingi Mia Moja katika kila kilo moja ya pamba itakayouzwa.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI