Friday, June 9, 2017

MFUMUKO WA BEI WA TAIFA WAPUNGUA HADI ASILIMIA 6.1

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO

MFUMUKO wa Bei wa Taifa kwa mwezi Mei, 2017 umepungua kwa asilimia 0.3,kutoka ule wa Mwezi April mwaka huu.
Mfumuko huo kwa bei ya Taifa,umepungua  hadi kufikia asilimia 6.1 kutoka asilimia 6.4 ilivyokuwa mwezi Aprili, 2017.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo amesema kupungua kwa mfumuko wa bei kunatokana na kupungua kwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwezi Aprili, 2017.
“Mfumuko wa Bei wa Taifa umepungua kutoka asilimia 6.4 kwa mwezi Aprili, 2017 hadi kufikia asilimia 6.1 kwa mwezi Mei , 2017 kutokana na kupungua kwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwezi Mei, 2017,” amesema Kwesigabo.
Kwesigabo amesema Mfumuko wa Bei wa mwezi Mei, 2017 unaopimwa kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa asilimia 0.2 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 0.5 ilivyokuwa mwezi Aprili, 2017.
Amesema Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi 109.26 kwa mwezi Mei, 2017 kutoka 109.04 mwezi Aprili, 2017 kutokana na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.
Kwesigabo ametaja bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi kuwa ni pamoja na mahindi yaliyoongezeka kwa asilimia 4.2, maharage mabichi kwa asilimia 2.9, maharage ya soya kwa asilimia 2.2, unga wa mtama kwa asilimia 1.5, viazi mviringo kwa asilimia 2.0, mihogo mikavu kwa asilimia 2.3, na magimbi kwa asilimia 2.5.
Aidha bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa fahirisi za bei ni pamoja na mkaa ulioongezeka kwa asilimia 2.5.
Ameongeza kuwa Mfumuko wa Bei kwa bidhaa za vyakula nyumbani na migahawani kwa mwezi Mei, 2017 umepungua hadi asilimia 11.8 kutoka asilimia 12.0 mwezi Aprili, 2017. Aidha, badiliko la Fahirisi za Bei kwa bidhaa zisizo za vyakula umepungua hadi asilimia 3.0 mwezi Mei, 2017 kutoka asilimia 3.4 mwezi Aprili, 2017.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI