SERIKALI imedai kupokea kwa
mshtuko,taarifa za kutoweka kwa Mwanamuziki,Ibrahim Mussa,almaarufu kwa jina la
Kisanii;“ Roma Mkatoliki.”
Katika taarifa yake,kupitia Wizara ya
Habari, Utamaduni, sanaa na Michezo imesema imepokea kwa mshtuko taarifa za
kutoweka kwa msanii huyo tangu tarehe 5 Aprili 2017, na kuomba wananchi
washirikiane na vyombo vya Dola,kuhakikisha anapatikana.
Taarifa hiyo ya Serikali,ilitolewa
jana jioni na kusainiwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa
wizara Zawadi Msall,imeeleza Wizara hiyo ambayo ndiyo inadhamana na tasnia ya
sanaa,imefuatilia kwa kina suala.
Imedai kwa kuwa tukio hilo lina
muelekeo wa jinai na kwamba kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo vya dola
vilivyothibitisha kutomshikilia katika kituo chochote cha Polisi,ni vyema
jitihada zikafanyika za kupatikana sambamba na wenzake.
Hivyo Serikali imewaomba wadau
mbalimbali na wananchi kwa ujumla kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa
taarifa zozote zitakazo saidia kujua alipo msanii huyo.
Roma Mkatoliki akiwa na wasanii
wenzake wawili,imedaiwa kutekwa wakiwa katika shughuli zao za kawaida za
kisanii katika studio,ambapo watekaji hao waliondoka na baadhi ya vifaa vya
studio.
Hili ni tukio la pili kubwa nchini
kutokea,baada ya hapo awali msaidizi wa masuala ya Kisiasa wa Mwenyekiti wa
Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo “CHADEMA”,Freeman Mbowe;aitwaye Ben
Sanane,kutoweka hadi leo hajulikani alipo.