MKUU wa Mkoa wa Mwanza,John
Mongella, amejitokeza na kudai vitendo vya uvuvi haramu vinavyoendelea
vinabarikiwa na baadhi ya baadhi ya Maafisa kwa
maslahi yao binafsi.
Uwepo wa Maafisa uvuvi hao wasio
waaminifu,wasiozingatia weledi wa majukumu yao,kutokana na kushirikiana na
wavuvi haramu,ni janga linaloiangamiza Taifa,anaandika Tunu Herman.
Mkuu huyo wa Mkoa anasema kitendo cha
Wavuvi kuendelea kuvua samaki kwa njia haramu kunachangiwa na Maafisa
Uvuvi,ambao huwakamata kisha huwaachia pasipo kuwachukulia hatua kali za
kisheria zenye maslahi ya Taifa.
Amesema vitendo vya kuwakamata kisha
kuwaachia bila sababu maalumu,linaipotezea Serikali Rasilimali nyingi
zinazotumika kupambana na tatizo hilo,ambazo zingeelekezewa katika kutatua
changamoto zinazo ikabili jamii.
Akiwa katika eneo la Mwalo wa
Kirumba,kufuatia tukio la kukamatwa kwa samaki kilogram 3482 wenye
thamani ya Shilingi Milioni 20,892,000/= waliovuliwa kinyume cha sheria na
kusafirishwa kwa njia ya magendo,anasema, vita hivyo haviwezi kufanikiwa ikiwa
Maafisa uvuvi wataamua kuendelea kushirikiana na Wavuvi hao haramu.
Anasema,"Kama Maafisa wa Serikali, wakiwa ndio vinara wakuwasaidia wavuvi haramu ni bora tukafanye kazi zingine, maana kama mtu anakamatwa na kuachiwa kwa ujanjaujanja kwa ajili ya Masilahi binafsi ambayo yanaleta madhara kwa wananchi na serikali kwa ujumla, hakuna haja ya kuwekeza nguvu kubwa katika mapambano hayo.”
“…haiwezekani kupambana kutokomeza Uvuvi haramu kuwe tatizo kwa
Serikali,kumbe kuna watu wananufaika,hawana
uchungu na maslahi ya Taifa,kwani wameendekeza
tamaa,pasipo kujali wanalipwa mshahara na serikali,inayotokana na kodi za
wananchi," alisema Mongella.
Aidha Mongella alimuagiza Mkuu wa Kituo cha Polisi Kirumba,Susan Kidiku na Kamanda wa Takukuru mkoani Mwanza, Ernest Makale,kumkamata na kumfanyia uchunguzi Ofisa wa Uvuvi wa wilaya ya Ilemela,Ivon Maha,aliyehusika kumkamata na kumuachia Mfanyabiashara aliyekamatwa na samaki zaidi ya tani tano.
Mfanyabiashara huyo,Mageta Bigamboa,alikamatwa
akitokea wilayani Ukerewe,akiwa na samaki zilizobebwa kwenye gari aina ya
Mistubishi Fuso lenye namba T 202 BGE ambalo ni mali ya Magireti Agustino.
Ameagiza hatua za kisheria zichukuliwe
kwa wakati,kutokana na mtumishi huyo wa serikali,kuchambua kisha kuruhusu tani
mbili za samaki kuondoka bila kibali cha chakusafirishia,huku
akitambua mhusika aliyemuidhinisha hakuwa na Leseni ya biashara.
Agizo hilo lilitolewa na Mongella,
kufuatia maelezo yakubabaisha yaliyotolewa na Afisa Uvuvi huyo kudai, kufuatia
kukamatwa kwa Samaki hao na Taasisi ya kupambana na rushwa wao kama
wataalam wa masuala ya samaki waliwachambua,kisha kubaini kilo 2,316 wenye thamani
ya Shilingi 13,896,000/- kukidhi viwango.
Afisa Uvuvi huyo anajitetea kwa kudai maamuzi hayo kuyatoa
kushirikiana na Maafisa wa TAKUKURU,kuruhusu samaki hao wachukuliwe na
mhusika,jambo ambalo linakanushwa vikali na Mkuu wa Takukuru mkoani Mwanza,mbele
ya Mkuu wa mkoa huyo.
"Mkuu wa Mkoa, sio kweli kwamba TAKUKURU, tullishiriki kuwaachia samaki hao walio chambuliwa, kwani sisi mara baada ya kuwatia mbaroni wahusika, tulichokifanya nikuwaita waatalaam wavuvi na kuwakabidhi samaki lakini tukaondoka na kibali husika kilichokuwa kinatumika kuwasafirishia samaki hao," alisema Mkuu wa Takukuru Mkoani Mwanza,Makale.
Mkoa wa Mwanza upo katika Mapambano ya vita dhidi ya Uvuvi haramu,tayari Nyavu za makila na Zana zingine za uvuvi haramu zimeisha kamatwa kwenye maeneo ya Buchosa, Ilemela, Sengerema na Ukerewe na kuteketezwa kwa Nyakati tofauti
Kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi namba 22 ya Mwaka 2003 na kanuni zake za Mwaka 2009 ni makosa kuvua samaki aina ya Sangara waliochini ya Sentimita 50 ambao wanatajwa kama samaki wachanga, pia inakataza kuvua samaki walio zaidi ya Sentimita 85, ambao huuchwa kwaajili ya mazalia ya Samaki.