Thursday, April 6, 2017

HOTUBA YA WAZIRI MKUU;KASSIM MAJALIWA BUNGENI;APRIL 6,2017.

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO

UTANGULIZI

  1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja kwamba kutokana na taarifa zilizowasilishwa leo katika Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2016/2017 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018. Aidha, ninaliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
  1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Bunge lako Tukufu limeondokewa na Wabunge wenzetu, Mheshimiwa Hafidh Ally Tahir aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Dimani – CCM na Mheshimiwa Dkt. Elly Marko Macha, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum – CHADEMA. Pia, Taifa lilimpoteza Mheshimiwa Samwel John Sitta aliyekuwa Spika Mstaafu wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, nchi yetu imekumbwa na majanga na maafa yaliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali. Ninaomba Mwenyezi Mungu awajalie nafuu ya haraka wale wote waliopata majeraha, na kuwapumzisha kwa amani wale waliopoteza maisha, Amina! Ninatoa pole kwa familia za wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki. Pia ninatoa pole kwa Mheshimiwa Aida Khenani aliyepata ajali ya kugongwa na pikipiki wakati akitoka Bungeni. Tunamuombea apone haraka na aweze kurejea Bungeni ili kuendelea na majukumu yake.

PONGEZI NA SHUKRANI

  1. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar kwa kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wao. Sisi tunaowasaidia tunajivunia uongozi wao mahiri, uzalendo uliotukuka na dhamira njema waliyonayo kwa Watanzania.
  1. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Bunge lako Tukufu limepokea na kuwaapisha Wabunge wapya watano, ambao ni Mheshimiwa Abdallah Majura Bulembo (Mb.), Mheshimiwa Anne Killango Malecela (Mb.), Mheshimiwa Juma Ali Juma (Mb.), Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb.) na Mheshimiwa Salma Rashidi Kikwete (Mb.). Ninawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wapya kwa heshima waliyoipata ya kujumuika nasi kwenye Bunge hili. Kama ilivyo ada, tutatoa ushirikiano unaotarajiwa kwa Waheshimiwa Wabunge hawa ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi na tija. Kipekee, ninampongeza Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Pia ninatumia nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote walioteuliwa kuingia kwenye Bunge la Afrika Mashariki, Makatibu Wakuu wapya walioteuliwa na Mheshimiwa Rais yaani Profesa Kitila Alexander Mkumbo, Dk. Leonard Akwilapo, Maimuna Tarishi na Dk. Ave Maria Semakafu. Nawapongeza sana wote walioteuliwa kushika nyadhifa hizo.
  1. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwashukuru Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kazi kubwa ya kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Ninawashukuru kipekee sana Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria inayoongozwa na Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni na Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini kwa kutoa mchango mkubwa wakati wa maandalizi ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Pia, niwapongeze Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kuongoza kwa umahiri mkubwa Kamati zao wakati wa kupitia makadirio ya sekta zote. Maoni na ushauri wao umesaidia sana kuboresha Makadirio ya Bajeti ya Serikali kwa mafungu yote.
  1. Mheshimiwa Spika, niruhusu pia niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wakuu wa Idara, Mashirika na Taasisi zote za Serikali kwa ushirikiano wanaoendelea kunipa katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, ninawashukuru Wafanyakazi wote wa Serikali na Taasisi zake chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi, kwa kukamilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/2018.
  1. Mheshimiwa Spika, kipekee, ninamshukuru Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama (Mb.), Mbunge wa Peramiho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu); Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde (Mb.), Mbunge wa Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana) kwa ushirikiano wao mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Aidha, ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Abdallah Possi aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa aliyofanya wakati akiitumikia nafasi hiyo. Ninamtakia kazi njema kwenye jukumu lake  jipya la kuiwakilisha Tanzania nchini Ujerumani. Vilevile, ninawashukuru wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya Uongozi wa Makatibu Wakuu, Dkt. Hamisi H. Mwinyimvua; Bwana Eric F. Shitindi na aliyekuwa Katibu Mkuu Bwana Uledi A. Mussa kwa ushauri wao wa kitaalam kwangu na kwa Waheshimiwa Mawaziri.
  1. Mheshimiwa Spika, ninazishukuru pia nchi marafiki, Taasisi na Mifuko ya Fedha Duniani, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Madhehebu ya Dini na Mashirika yasiyo ya Kiserikali kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kujenga uchumi wa nchi yetu. Misaada na mikopo iliyopatikana kwa wakati imechangia kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
  1. Mheshimiwa Spika, ninapenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati wananchi wa Jimbo la Ruangwa kwa kuendelea kuniunga mkono na kuielewa vizuri dhamana ya Kitaifa niliyonayo ya kusimamia utendaji wa Serikali katika sekta zote na kuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni. Mwisho ninaishukuru familia yangu hususan mwenza wangu mpendwa, Mary na watoto wetu kwa upendo, dua na kuendelea kunitia moyo ili nitekeleze kwa ufanisi zaidi majukumu yangu ya Kitaifa. Asanteni sana!

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI