HALMASHAURI
ya Mji wa Kahama imemsimamisha Kazi,Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili,Joachim
Henjewele,huku ikiwataka watumishi wengine watatu
katika Idara hiyo kujieleza
kutokana na tuhuma zinazowakabili juu ya kukithiri kwa migogoro ya Ardhi Mjini
Kahama.
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Mji wa Kahama,Anderson Msumba,alisema Henjewele alisimamishwa
kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili za kushindwa kuwajibika ipasavyo
kwenye idara hiyo na kuwa chanzo cha migogoro ya Ardhi.
Msumba
alisema mbali na Halmashauri kumsimamisha Mkuu huyo wa idara pia imewaandikia
barua ya kujieleza kwanini wasichukuliwe hatua,maafisa watatu katika Idara hiyo
ambao ni Ofisa Mipango Miji; Irene Maro,Ofisa ardhi mpimaji Yahaya Msangi na
afisa ardhi katika halmashauri hiyo,Yusuph Luhumba.
Maamuzi
hayo ya Halmashauri yamechukuliwa kufuatia
Kamati ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkurlu,iliyoundwa mwishoni
mwa mwaka jana na kuongozwa na Ofisa Tawala wake;Said Yasini,kuchunguza
migogoro ya ardhi kwenye Halmashauri ya Mji wa Kahama,kubaini ukiukwaji mkubwa
katika suala la upimaji wa viwanja kwenye maeneo mbalimbali ya mji huo .
Kufuatia
ripoti hiyo,Mkuu wa Wilaya ya Kahama,alitoa agizo katika Baraza la Madiwani la
Halmashauri hiyo,kuwachukulia hatua watumishi wote waliohusika kuvuruga upimaji
wa viwanja hivyo ikiwa ni pamoja na kufanya uchunguzi kwenye makampuni
yaliyokuwa yakihusika na zabuni ya upimaji wa viwanja hivyo.
Hata
hivyo Henjewele,ambaye yupo likizo alipoongea na mwandishi wa habari hii alipingana
na Mkurugenzi wake kwamba amesimamishwa kazi,bali alikiri kupokea barua ya
kujieleza aliyoipata akiwa mapumzikoni.
Kwa
upande wa Umoja wa Wazee wa wilaya ya Kahama (UWAKA),umedai kutoridhishwa na
hatua hizo zilizochukuliwa kwa watu wachache huku idara nzima ikiwa haiwajibiki
ipasavyo na kusababisha kuibuka kwa mogogoro ya viwanja mara kwa mara..
Katibu
UWAKA, Paul Ntelya,alisema umoja huo unaona hatua zilizochukuliwa pamoja na kuwakumba
baadhi ya vigogo katika Idara ya Ardhi,lakini hazijagusa vinara wa
migogoro,ambao baadhi yao wakisalimika
pasipo hata kupewa onyo huku wakihusika na kuuza maeneo mengi,mjini
Kahama,likiwemo la Nyahanga.
“Tunajiuliza
kwanini aliyehusika kuuza eneo Nyahanga ambalo limejengwa maghala licha ya
mmiliki wake kuzuiwa,kwakuwa ni eneo la Shule ya Msingi Nyahanga,lakini
pamejengwa,na aliyehusika kuuza eneo hilo wakishindwa kumchukulia
hatua,”alisema Ntelya.