Tuesday, February 21, 2017

SOKA LA WANAWAKE KUTAMALAKI WILAYANI KAHAMA.

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO




IMEELEZWA kwamba mpango wa kutoa mafunzo ya michezo kwa walimu wa shule za msingi,sekondari na jamii unaoendeshwa na Mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu,uliopo wilayani Kahama,unaomilikiwa na Kampuni ya ACACIA,utasaidia kukuza soka la wanawake nchini.

Hayo yalielezwa na Mwalimu wa Michezo katika Shule ya Msingi Kakola B,Sophia Manganda Mang’erere,kwa kueleza kuwa fursa waliyopata ya kuhudhuria kozi ya michezo ikijumuisha soka inayotolewa na klabu ya Sunderland ya Uingereza chini ya ufadhili wa Mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu,utasaidia kukuza soka la wanawake.

Alisema soka la wanawake limekuwa halipigi hatua nchini kutokana na walimu wa mchezo huo kuwa wanaume,jambo lisiloleta mazingira rafiki kwa wanawake kuucheza,lakini kutokana na sasa kupatikana kozi za walimu wa kike katika soka kutasaidia kuleta hamasa zaidi kwa watoto wa kike kucheza mchezo huo.

“Nashukuru kampuni ya ACACIA kupitia Mgodi wake wa Bulyanhulu,kuona umuhimu wa kukuza soka la wanawake kwa kuwashirikisha walimu wa kike kuhudhuria kozi ya mchezo huo,hii itarahisisha kupatikana hamasa kwa wanawake kuupenda mchezo wa soka katika wilayaya Kahama,ambao upo nyuma kwa soka la wanawake,”alisema Mang’erere.

Aidha alisema atatumia kozi aliyoipata kuhamasisha wasichana mashuleni kushiriki soka la wanawake na kuwapatia mafunzo ya msingi wa mchezo huo sambamba na mpira wa pete,huku akiomba ngazi zinazohusika kuboresha soka la wanawake kwa kuanzisha mashindano mbalimbali toka ngazi ya mashuleni,kata,wilaya,mkoa sambamba na ligi Kuu ya soka la wanawake.

Kwa upande wake Mwalimu wa jamii wa michezo ya Kandanda na mpira wa pete,John Machimu,alisema kozi hiyo imemsaidia kuboresha taaluma yake hiyo,ambayo ataitumia kuibua vipaji vya michezo hiyo kwa kutoa mafunzo yaliyokidhi vigezo vya kitaaluma,hatua itakayosaidia kupata wanamichezo watakaokuwa na tija kwa Taifa.

Nae Kiongozi wa Michezo katika Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu,Charles Mwandindi,alisema lengo la mafunzo hayo ni kusaidia walimu wa michezo hiyo kuwa na utaalamu unaokubalika na ngazi ya michezo ya Taifa,ili kusaidia kukuza vipaji vitakavyosaidia kupata wachezaji ambao watapeperusha vyema bendera ya Taifa katika michezo hiyo.

Mwandindi alisema mpango huo wa kuwapatia mafunzo walimu wa michezo utakuwa wa miaka miwili,utakaoshirikisha walimu 59 wa michezo hiyo,ambapo miongoni mwake wanawake ni 14,kati yao sita ni kutoka Shule za Misingi na nane kutoka katika Jamii.

Alisema katika mafunzo hayo yaliyotolewa na mwalimu wa michezo kutoka timu ya Sunderland ya Uingereza,yalihusisha walimu wa michezo kutoka Halmashauri ya Msalala,wilayani Kahama na Nyanghw’ale toka wilayani Nyanghw’ale,na yalikuwa ya hatua ya awali huku hatua ya pili ikitarajia kuanza mwezi Mei mwaka huu.

 Alibainisha kwamba mafunzo hayo kwa mchezo wa soka washiriki wake wamepata leseni daraja D inayotambulika na TFF,yalijumuisha walimu wa kiume kutoka katika jamii 28,wanne kutoka Shule za Sekondari na wanaume kumi kutoka shule za msingi na maafisa michezo watatu kutoka kila wilaya.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI